Jul 02, 2022 02:20 UTC
  • Idadi ya Wamarekani wanaotaka kubeba silaha dhidi ya serikali yafichuliwa

Utafiti mpya wa maoni unaonesha kuwa, akthari ya wananchi wa Marekani wanajiona kama wageni ndani ya nchi yao, na kwamba baadhi yao wanasema wako tayari kufanya ghasia na kutumia silaha dhidi ya serikali hiyo.

Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Chicago umefichua kuwa, aghalabu ya Wamarekani wanaitazama serikali ya nchi hiyo kama taasisi fisadi, ambayo inafanya kazi dhidi ya maslahi ya wananchi.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 49 ya watu waliohojiwa wanasema kadri siku zinavyopita, ndivyo wanavyojihisi kuwa wageni ndani ya nchi yao,  huku aghalabu ya wenye mtazamo huu wakiwa wafuasi wa chama cha Republican na wahafidhina.

Utafiti huo umesema, katika kila Wamarekani wanne, mmoja anahisi kuwa serikali haiwatendei haki wananchi, na wanasema karibuni hivi huenda watalazimika kubeba silaha dhidi ya serikali yenyewe.

Kwa ujumla, asilimia 28 ya Wamarekani walioshirikishwa kwenye utafiti huo wamesema kuna muda utafika watalazimika kubeba silaha na kutumia mbinu za fujo mkalaba wa serikali. 

Bunduki zinavyouzwa kama pipi madukani nchini Marekani

Asilimia 38 ya wanaokubaliana na wazo hili ni wahafidhina, asilimia 36 wafuasi wa chama cha Republican, asilimia 35 miongoni mwao ni wale ambao hawaungi mkono chama chochote cha kisiasa, huku asilimia 37 wakiwa wale wanaomiliki bunduki na silaha moto.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Chicago, asilimia 19 ya Wademocrat wanaodai kuwa na 'misimamo laini' wanasema mapambano ya silaha huenda yakawa ya lazima nchini Marekani katika kipindi kifupi kijacho.

Tags