Jul 02, 2022 07:56 UTC
  • Papa Francis
    Papa Francis

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani ametangaza kuwa Umoja wa Mataifa "hauna uwezo" wa kutatua mgogoro wa vita nchini Ukraine.

Akizungumzia kushindwa kwa Umoja wa Mataifa kusitisha vita nchini Ukraine, Papa Francis amesema kuwa umoja huo hauna uwezo wa kutekeleza mamlaka yake, na kwamba ingawa unaweza kusaidia kuzuia vita, lakini hauwezi kuvisimamisha.

Papa Francis amesema sheria za Umoja wa Mataifa haziipi uwezo huo jumuiya hiyo. Amesisitiza katika mahojiano yake na gazeti la Italia la Corriere della Sera kwamba "hakuna irada na nia ya kuimarisha amani."

Ukraine

Kufuatia sera za serikali yenye mielekeo ya Magharibi ya Kiev na harakati za hivi karibuni za nchi wanachama katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharini (NATO) za kutaka kujipanua Mashariki mwa dunia hususan karibu na mpaka wa Russia, Rais wa nchi hii, Vladimir Putin, mnamo Februari 24, aliamuru operesheni maalumu ya kijeshi katika mkoa wa Donbas akijibu ombi la msaada wa kijeshi kutoka kwa wakuu wa jamhuri za Donetsk na Luhansk huko mashariki mwa Ukraine.

Rais wa Russia pia amelaani "sera za kupenda makuu" za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), ambalo anaamini linalenga kuimarisha "ubeberu" wake kupitia vita vya Ukraine.