Jul 02, 2022 09:11 UTC
  • Siasa za kundumakuwili za Wamagharibi katika mgogoro wa Ukraine

Vita vya Ukraine vimeingia katika mwezi wake wa tano. Siasa za kundumakuwili za Wamagharibi kuhusu mgogoro huo hadi sasa zimesababisha mdororo mkubwa wa uchumi, ungezeko kubwa la umasikini katika mamilioni ya familia duniani, vifo vya makumi ya watu na vilevile kusababisha mamilioni ya watu huko Ukraine kuwa wakimbizi.

Kupungua akiba ya mafuta ya kimkakati ya Marekani hadi kufikia kiwango cha chini zaidi katika miaka 40 iliyopita, ongezeko la mfumuko wa bei nchini Ufaransa, mpango wa Uingereza wa kusimamisha gesi inayotumwa Ulaya kupitia nchi hiyo, kuongezeka ukosefu wa ajira nchini Ujerumani sambamba na kuongezeka nchini wimbi la wahamiaji wa Kiukrani na kukamatwa mateka askari elfu 6 wa Ukraine na wanajeshi wa Russia ni baadhi tu ya vichwa muhimu vya habari ambazo zimekuwa zikitangazwa katika kipindi cha siku mbili zilizopita kuhusu mgogoro wa Ukraine na taathira zake kwa nchi za Magharibi.

Utegemezi wa nchi za Magharibi kwa gesi na mafuta ya Russia sasa umeingia katika hatua mpya. Kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Nishati ya Marekani, Hifadhi ya Kimkakati ya Petroli ya Marekani (SPR) ilipungua kwa mapipa milioni 6.9 katika wiki iliyoishia Juni 24, ambacho ni kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu Aprili 1986. Matukio hayo ni changamoto mpya kwa utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye serikali yake imekuwa ikijaribu kutumia mbinu tofauti kupunguza bei ya petroli, ikiwa ni pamoja na kuruhusu kutumiwa mafuta yasiyosafishwa kutoka hifadhi ya kimkakati ya mafuta ya Marekani.

Askari vitani Ukraine

Siku hizi, watu wa Marekani wamebadili maoni yao kuhusu mgogoro wa Ukraine baada ya kupanda bei ya petroli hadi kufikia dola 5 kwa geloni moja, ambacho ni kiwango cha juu zaidi cha bei ya mafuta kuwahi kushuhudiwa katika historia ya karibuni ya Marekani. Kwa mujibu wa uchunguzi wa kura ya maoni, 51% ya Wamarekani waliounga mkono siasa za nchi yao kuhusu mgogoro wa Ukraine mwezi Mei, sasa wamebadili mawazo yao kuhusiana na mzozo huo.

Katika upande wa pili, mgogoro wa Ukraine ambao umesababisha matatizo mengi ya nishati duniani umeifanya Uingereza ithibitishe kuwa haitofautishi kati ya adui na rafiki wakati wa mgogoro. Gezeti la Financial Times linalochapishwa mjini London karibuni hivi na baada ya kuongezeka mgogoro wa gesi barani Ulaya baada ya kuharibika uhusiano wa nchi za bara hilo na Moscow, liliandika kwamba, iwapo mgogoro wa gesi utaendelea Uingereza itafunga bomba linalosafirisha gesi ya Russia kuelekea Ulaya.

Licha ya kuwepo taathira haribifu za vita vya Ukraine kwa nchi za Magharibi lakini Rais Biden wa Marrekani siku ya Alkhamisi tarehe 30 Juni alitangaza habari ya kualikwa rasmi nchi za Sweden na Finland zijiunge na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi Nato. Alisema: 'Katika siku zijazo, tutatuma nchini Ukraine silaha mpya zenye thamani ya dola milioni 800.' Borris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza na bila kuashiria ughali mkubwa wa maisha unaoshuhudiwa nchini kwake pia amesema kuwa serikali ya London itaipa Ukraine msaada zaidi wa kijeshi wa pauni bilioni moja. Msaada huo utaifanya Uingereza kuwa nchi ya pili inayotoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine baada ya Marekani.

John Mearsheimer, mhadhiri wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Chicago amesema kuwa mzozo wa hivi sasa huko Ukraine umesababishwa na Marekani ambayo inataka kuiona nchi hiyo ya Ulaya ikiwa ngome ya nchi za Magharibi katika mpaka wa Russia na kuonya kwamba historia itakuwa na matokeo machungu kwa Marekani na waitifaki wake wa Ulaya kutokana na siasa za kipumbavu ambazo wanazitekeleza huko Ukraine.

Siasa za kundumakuwili ambazo zimekuwa zikitekelezwa na nchi za Magharibi kuhusiana na watu wa Ukraine pia hazijakuwa na matunda yoyote mazuri kwa nchi hizo. David Arakhamia, mkuu wa timu ya Ukraine inayofanya mazungumzo na Russia, hivi karibuni alikiri kwamba kila siku jeshi la nchi yake hupata hasara ya watu karibu elfu moja (waliouawa na kujeruhiwa) ambapo waliouawa huwa ni kati ya watu 200 hadi 500. Mbali na hayo maisha magumu ya mamilioni ya wakimbizi wa Ukraine pia ni suala linalotia wasiwasi.

Hasara ya vita Ukraine

Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa nchi za Magharibi zinamwaga pesa na silaha nchini Ukraine na kuiunga mkono kisiasa na kidiploamasia nchi hiyo kwa ajili ya kuishughulisha Russia na vita visivyo na maana. Kwa hakika inasikitisha kuona kwamba walimwengu wakiwemo Wamarekani na watu wa Ulaya wamelazimika kugharamia vita vya kichochezi na vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia kutokana na siasa mbovu zinazotekelezwa na wanasiasa wa Magharibi huko Ukraine.