Jul 02, 2022 11:47 UTC
  • Ilhan Omar: Minnesota ina machafuko makubwa zaidi kuliko kambi ya wakimbizi Wasomali ya Dadaab

Mbunge Muislamu mwenye asili ya Somalia anayewakilisha jimbo la Minnesota katika Baraza la Wawakilishi Marekani amesema, kiwango cha machafuko ya kutumia silaha moto katika jimbo hilo ni kikubwa zaidi kuliko cha kwenye kambi ya wakimbizi Wasomali aliyokuwa akiishi zama za utotoni.

Ilhan Omar ambaye alikuwa akihutubia hadhara ya watu wa jimbo lake kuhusiana na machafuko na mapigano ya utumiaji silaha moto yaliyoigubika Marekani, amesema, hali ya usalama ya mji wa Minnesota ni mbaya zaidi kuliko ya kambi ya wakimbizi aliyokuwa akiishi wakati alipokuwa mdogo.

Ilhan Omar amefafanua kwa kusema: "kwa muda wa miaka minne niliyokaa kwenye kambi Dadaab kwenye mpaka wa pamoja wa Somalia na Kenya, sikuwahi kushuhudia machafuko yoyote mpaka tulipokuja Minnesota".

Mbunge huyo wa jimbo la Minnesota kwa tiketi ya chama cha Democratic ameendelea kueleza kwamba,"katika mwaka wa kwanza na wiki tatu baada ya mimi na baba yangu kuwasili Minneapolis nilishuhudia mtu mmoja akiuliwa kwa kupigwa risasi; na miezi sita baadaye nikawashuhudia askari polisi wa Minneapolis wakimmiminia risasi 38 mhamiaji Msomali mwenye ulemavu wa akili ambaye hakuweza kuongea Kiingereza.

Aidha, Ilhan Omar amesema, katika muda alioishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Dadaab, watoto wadogo walikuwa wakienda skuli wakiwa wamebeba bunduki lakini hakukuwa na machafuko kama ya Minnesota.

Tangu ulipoanza mwaka huu wa 2022 hadi sasa, mji wa Minneapolis peke yake umeshasajili matukio 45 ya mauaji.  Mapema mwezi uliopita wa Juni viongozi 10 wa mifumo ya huduma za afya katika mji huo walitangaza machafuko ya utumiaji silaha moto kuwa ni mgogoro wa afya ya jamii.../