Jul 03, 2022 11:20 UTC
  • Jeshi la Russia lakomboa Donbass, askari wa Ukraine watimuliwa kikamilifu

Jeshi la Russia limetangaza mafanikio makubwa ya kuwatimua askari wa Ukraine kutoka Jamhuri ya Watu wa Luhansk, eneo ambalo limetangaza kujitenga na Ukraine.

Wizara ya Ulinzi wa Russia imetangaza kuwa eneo lote la Donbass limekombolewa na kuongeza kuwa leo Jumapili, Waziri wa Ulinzi Sergey Shoigu ameshamfahamisha Rais Vladimir Putin kuhusu mafanikio hayo.

Televisheni ya Russia imewaonyesha wanamgambo wa Luhansk wakiwa wanashangilia ushindi huo ambapo wamekuwa wakishirikiana na jeshi la Russia kuwatimua askari wa Ukraine.

Tarehe 24 Februari mwaka huu Rais Vladimir Putin aliamuru mashambulizi ya kijeshi katika eneo la Donbas akijibu ombi la msaada wa kijeshi kutoka kwa Marais wa Jamhuri za Donetsk na Luhansk. Hatua hiyo ya Putin ilichukuliwa sanjari na maombi ya mara kwa mara ya Ukraine ya kujiunga na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) na baada ya nchi hiyo kupokea msaada wa mamilioni ya dola kutoka nchi za Magharibi. 

Huko nyuma mwaka wa 2014, mikoa ya Donetsk na jirani yake Luhansk-ambazo kwa pamoja zinaunda Donbass-zilijitangaza kuwa jamhuri huru, zikikataa kutambua serikali ya Ukraine inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi wa NATO.

Hivi karibuni Rais Putin, alilaani "sera za kupenda makuu" za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), ambalo anaamini linalenga kuimarisha "ubeberu" wake kupitia vita vya Ukraine.

Putin ameutaja uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya kwa Ukraine kwa ajili ya kuendeleza vita na kupinga mazungumzo kuwa unathibitisha na kusadikisha mtazamo wake, akisema kwamba lengo la Wamagharibi na NATO si kulinda maslahi ya Ukraine na watu wake, bali ni kutetea maslahi yao binafsi. 

 

Tags