Jul 04, 2022 07:01 UTC
  • Kumbukumbu ya kushambuliwa ndege ya abiria ya Iran; jinai isiyosameheka ya Marekani

Jana tarehe 3 Julai ni siku ya kumbukumbu ya shambulio la kombora lililofanywa na meli ya kivita ya Marekani ya Vincennes dhidi ya ndege ya abiria ya Iran aina ya Airbus iliyokuwa ikiruka kutoka Bandar Abbas kuelekea Dubai.

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo (Julai 3, 1988), abiria wote 290, wakiwemo watoto 66 na wanawake 53, waliuawa kinyama kutokana na uamuzi uliochukuliwa na nahodha wa manowari ya Vincennes wa kutungua kwa kombora ndege hiyo ya abiria ya Iran. Kati ya abiria hao, 254 walikuwa Wairani, 13 raia wa Umoja wa Falme za Kiarabu, kumi walikuwa Wahindi, sita Wapakistani, sita raia wa Yugoslavia na mmoja Mwitaliano.

Baada ya kutunguliwa ndege hiyo, viongozi wa Marekani walitoa sababu zilizogongana wazi za kujaribu kuhalalisha jinai hiyo usiyosameheka na kuonyesha kuwa kitendo hicho cha uadui kilifanyika kimakosa, lakini kwa kuzingatia kwamba meli ya vita ya Vincennes ilikuwa na vifaa na mifumo ya kisasa kabisa ya rada na pia kutambulika wazi ndege iliyokuwa angani, ilibainika wazi kuwa hakukuwepo na uwezekano wa kufanyika kosa katika mazingira hayo na kwamba hiyo ilikuwa hatua iliyochukuliwa kwa makusudi na adui kwa madhumuni ya kusababisha maafa na hasara dhidi ya taifa la Iran.

Monawari ya Vincennes na kamanda wake Admeri William Rogers

Katika kutapatapa kwao, Wamarekani walishindwa kutoa hoja ya kimantiki ya kuhalalisha kitendo hicho cha jinai. Kwanza, walidai kuwa ndege hiyo ilikuwa ya kijeshi, kisha wakasema ilikuwa ikipaa nje ya njia yake ya kawaida angani, na baada ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na Jumuiya ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (IATA), kuthibitisha kuwa ilikuwa katika njia sahihi ya usafiri, wakadai kuwa walifananisha kimakosa ndege hiyo na ile ya kivita ya F14. Jambo la kushangaza na lililothibitisha kuwa viongozi wa Marekani walikuwa wanasema uongo ni kwamba waliamua kumtunuku kamanda wa Vincennes medali ya ushujaa kutokana na jina hiyo.

Ukweli ni kwamba kuna orodha ndefu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani, na uungaji mkono wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa nchi hiyo kwa wavunjaji wakuu wa haki za binadamu na tawala za mauaji ya watoto ukiwemo utawala wa Kizayuni ni ukweli ambao haufichiki mbele ya fikra za waliowengi ulimwenguni.

Mbali na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia iliwasilisha malalamiko yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu huko The Hague, lakini ikiwa chini ya ushawishi na mashinikizo ya kisiasa ya Marekani, ICAO, badala ya kufanya uchunguzi wa kiufundi na kuwasilisha matokeo yake kwa Baraza la Usalama, ilitosheka tu kwa kuelezea masikitiko na kutuma salamu za rambirambi kwa familia na wafiwa wa ukatili huo wa Marekani.

Katika kueleza ni kwa nini Wamarekani walitekeleza jinai hiyo kwa kuiangusha ndege ya abiria, ni muhimu kutaja vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam dhidi ya Iran, vita ambavyo viliendeshwa kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani. Kwa kweli, mchakato na mkondo wa vita hivyo haukuwafurahisha  viongozi wa Marekani. Kwa maneno mengine ni kwamba awali viongozi hao walidhani kuwa vita hivyo vingefikia malengo yao katika kipindi kifupi, lakini badala yake mapambano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa Iran katika medani za vita ulizuia utekelezwaji wa matakwa ya nchi hiyo ya Magharibi katika vita hivyo.

George Shultz, Waziri wa Mambo ya Nje katika utawala wa  Ronald Reagan mnamo 1986, alisema katika hotuba yake mbele ya jumuiya ya Wazayuni wa Marekani kwamba: "Hatari katika Ghuba ya Uajemi ni kubwa na ya kweli. Ikiwa Ukhomeini utaenea katika eneo, bila shaka maslahi ya kimkakati ya Marekani yatadhurika, na ni wazi kuwa, maslahi ya Israel pia yatadhurika."

Ghuba ya Uajemi

Kwa msingi huo, Manowari ya Vincennes chini ya unahodha wa Admeri William Rogers, iliamriwa kutoka kwenye bandari ya San Diego, kwenda  Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya kuzishinikiza meli za mafuta za Iraq ambapo hatimaye ilihusika katika jinai ya kutisha ya kuwaua kinyama raia wote 290 waliokuwa kwenye ndege ya abiria ya Iran. Jinai hiyo ilitekelezwa kwa lengo la kulifanya eneo la Ghuba ya Uajemi kuonekana kuwa lisilo salama, na pia kudhoofisha uchumi wake ambao unategemea mafatu na wakati huo huo kuuimarisha utawala wa Saddam katika vita vilivyoanzishwa dhidi ya Iran.

Ni wazi kwamba kutunguliwa ndege ya abiria ya Iran na manowari ya Marekani katika Ghuba ya Uajemi na kuuawa shahidi abiria wake ni moja ya maafa yasiyosahaulika katika historia ya mwanadamu na aibu ya milele kwa wale wanaodai kutetea haki za binadamu duniani.  Bila shaka jinai hiyo iliyosababisha majeraha makubwa yasiyopona kwenye nyoyo za wapigania uhuru na ukweli ulimwenguni, ilithibitisha kwamba Marekani ambayo inadai kutetea haki za binadamu na kupambana na ugaidi duniani, yenyewe ni miongoni mwa wavunjaji wakubwa wa haki za binadamu na mmoja wa waungaji mkono wakuu wa ugaidi kimataifa.