Jul 04, 2022 07:38 UTC
  • Maandamano Marekani baada ya polisi kumuua kijana Mwafrika-Mmarekani

Maelfu ya waandamanaji waliokuwa na hasira waliingia barabarani katika jimbo la Ohio, katikati mwa Marekani siku ya Jumapili kulaani kitendo cha polisi kumuua kikatili kijana mwenye asili ya Kiafrika ambaye hakuwa na silaha.

Maandamano hayo yameitishwa baada ya kusambaa klipu za video zinazoonyesha uhalifu huo wa kishetani.

Klipu hizo za kuogofya zilionyesha maafisa wanane wa polisi wakihusika katika ufyatuaji risasi uliomuua Jayland Walker baada ya kutosimama katika taa za barabarani mnamo Juni 27 katika jiji la Akron huko Ohio. Kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 25 alipigwa na angalau risasi 60 kwa kosa tu la kutosimamisha gari kwa mujibu wa ishara za mataa ya barabarani.

Siku ya Jumapili, waandamanaji wenye hasira walirudi kwenye mitaa ya Akron, kwa siku ya nne mfululizo wakiandamana hadi makao makuu ya jiji huku wakiwa wamebeba mabango yenye kauli mbiu kama vile "Uadilifu kwa Joyland."

Baada ya awali kutoa maelezo mafupi kuhusu kifo cha Walker, maafisa wa Akron hatimaye walitoa video mbili siku ya Jumapili ambazo zilijumuisha video kamili ya tukio hilo ambalo lilirekedowa na kamera ambazo polisi huwa nazo kwenye sare zao.

Kulingana na video hizo, polisi walianza kukakbiliana na Walker kwa kulifuata gari lake kwa kasi kutokana na kitendo chake cha kutosimama katika mataa ya barabarani.

Jayland Walker

Baada ya kukimbizwa kwa dakika kadhaa, gari la Walker hatimaye lililazimika kusimama katika eneo la kuegeshea magari. Maafisa wa polisi wamedai kuwa kijana huyo ambaye hakuwa na silaha alifanya harakati ambazo zilipelekea waamini kuwa alikuwa anakusudia kuwapiga risasi.

Video zinaonyesha maafisa wote wa polisi waliokuwepo eneo la tukio wakimfyatulia risasi Walker, na kumpiga risasi mara kadhaa mfululizo na hivyo kutangazwa kufariki papo hapo.

Kumekuwa na msururu wa vitendo vya polisi ya Marekani kuwaua kiholela Wamarekani wenye asili ya Afrika katika majimbo tofauti ya nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni, na kusababisha maandamano makubwa.

Ukatili huo uliongezeka maradufu wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye mara kwa mara alijihusisha na maneno ya ubaguzi wa rangi.