Jul 04, 2022 14:09 UTC
  • Waziri Mkuu Uhispania: Morocco inapaswa kulaumiwa kwa maafa ya wahajiri wa Kiafrika, Melilla

Waziri Mkuu wa Uhispania amesema kwamba mkasa wa wahajiri wa Kiafrika katika eneo la Melilla unapaswa kuchunguzwa nchini Morocco na kwamba ni serikali ya Rabat ambayo inapaswa kuwajibika katika suala hili.

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez amesisitiza kwamba suala la ukiukwaji wa haki za binadamu katika mkasa wa Melilla mnamo Juni 24, ambapo wahamiaji wasiopungua 23 waliuawa, unapaswa kuzungumzwa huko Rabat.

Kuhusu picha zilizochapishwa za janga hilo na haja ya kuheshimiwa haki za binadamu katika hali hiyo, Sánchez amesisitiza kuwa: "Ni serikali ya Morocco ambayo inapaswa kujibu swali hili. Tunawajibika kuzungumzia kuhusu tunachokifanya nchini Uhispania."

Kwa mujibu wa maafisa wa Morocco, wahamiaji wasiopungua 23 wa Kiafrika kati ya jumla ya wahajiri wapatao 2,000 waliokuwa wakijaribu kuingia eneo la Melilla, walifariki dunia tarehe 24 Juni. Hata hivyo taasisi zisizo za serikali zinasema idadi ya wahajiri wa Kiafrika walioaga dunia katika mkasa huo ni kubwa zaidi. 

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa mauaji ya makumi ya wahajiri wa Kiafrika katika mpaka wa Morocco na Uhispania.

Moussa Faki Mahamat

Moussa Faki Mahamat alieleza kuwa ameshtushwa na tukio hilo la kuuawa Waafrika 23, huku makumi ya wengine wakijeruhiwa wakijaribu kuvuka mpaka wa kimataifa kutoka Morocco kwenda Uhispania.

Mahamat amesisitizia haja ya kufanywa uchunguzi huru haraka iwezekanavyo, sambamba na kutoa mwito kwa nchi za dunia kutekeleza wajibu wao wa kuheshimu utu, heshima na usalama wa wahajiri, kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Siku hiyo, wahajiri karibu 2,000 wengi wao wakiwa raia wa Sudan walijaribu kuruka uzio wa vyuma na kuingia katika eneo la Melilla linalodhibitiwa na Uhispania kaskazini mwa Morocco, lakini wakakabiliwa kwa mkono wa chuma na maafisa usalama wa Morocco na Uhispania.

Tags