Jul 05, 2022 01:01 UTC
  • Marekani yakumbwa na wasiwasi wa kushadidi ghasia baada ya mauaji ya Jayland Walker

Maafisa wa serikali ya Marekani wameelezea wasiwasi wao juu ya kuongezeka maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi baada ya mauaji ya kijana mweusi huko Ohio na vilevile ghasia zinazosababishwa na mauaji hayo.

Gazeti la Los Angeles Times limeandika katika ripoti yake kwamba kufuatia mauaji yaliyofanywa na polisi dhidi ya Jayland Walker, Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyekuwa na umri wa miaka 25, na wasiwasi kwamba maandamano ya kupinga mauaji ya raia huyo yatasababisha vurugu kubwa, kuna uwezekano wa kufutwa sherehe za tarehe 4 Julai kwa kuchelea machafuko na mapigano kati ya raia na polisi.

Maelfu ya waandamanaji waliokuwa na hasira walimiminika barabarani katika jimbo la Ohio, katikati mwa Marekani siku ya Jumapili, kulaani kitendo cha polisi kumuua kikatili kijana mwenye asili ya Kiafrika ambaye hakuwa na silaha. 

Video za kuogofya zilionyesha maafisa 8 wa polisi wakihusika katika ufyatuaji risasi uliomuua Jayland Walker baada ya kutosimama katika taa za barabarani mnamo Juni 27 katika jiji la Akron huko Ohio. Kijana huyo alipigwa risasi zisizopungua 60 kwa kosa tu la kutosimamisha gari kwa mujibu wa ishara za mataa ya barabarani! 

Jayland Walker

Kumekuwepo msururu wa vitendo vya polisi ya Marekani kuwaua kiholela Wamarekani wenye asili ya Afrika katika majimbo tofauti ya nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni, na kusababisha maandamano makubwa.

Ukatili huo uliongezeka maradufu wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye mara kwa mara alijihusisha na maneno ya ubaguzi wa rangi.

Ubaguzi na ukiukwaji wa haki za watu weusi huko Marekani umekita mizizi katika kihistoria ya nchi hiyo kiasi kwamba rais wa zamani wa Marekani Barack Obama aliwahi kusema kuwa: "Ubaguzi wa rangi uko katika DNA ya Wamarekani." 

Tags