Jul 06, 2022 07:02 UTC
  • Marekani yafumbia macho ukweli kuhusu mauaji ya Shireen Abu Akleh

Licha ya kuwepo ushahidi na dalili za wazi kuhusu mauaji ya Shireen Abu Akleh, mwandishi ya televisheni ya al-Jazeera ya nchini Qata, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa taarifa ikidai kwamba mauaji hayo hayakuwa ya makusudi.

Hii ni katika hali ambayo mauaji hayo yalitekelezwa mbele ya macho ya mamilioni ya walimwengu na bila shaka uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani wa kutoa taarifa ya aina hiyo ni dharau na kukejeliwa wazi hisia za mamilioni ya watu duniani.

Kama tathmini ya aina hiyo ingetolewa na serikali ya Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani hilo halingekuwa jambo la kushangaza sana, lakini suala ambalo limeibua maswali mengi ni kuwa taarifa hiyo imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya chama cha Demokrasia cha Rais Joe Biden, ambaye amekuwa akitoa ahadi na madai mengi kuhusu nia yake ya kutetea uhuru wa waandishi na vyombo vya habari. Taarifa hiyo kwa mara nyingine imethibitisha ukweli kwamba, serikali ya Biden inafuata siasa zile zile zilizofuatwa na serikali ya Trump kuhusu utawala ghasibu wa Israel. Ni wazi kuwa Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani huko nyuma pia aliwahi kuthibitisha kivitendo ukweli huo.

Mazishi ya Abu Akleh

Kwa msingi huo ni wazi kuwa taarifa iliyotolewa karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu kutokuwa ya makusudi mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari wa televisheni ya al-Jazeera, imetolewa kimaslahi na kinyume na matamshi ya kipropaganda yaliyotolewa na chama cha Demokrasia kuwa kinaunga mkono uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari.

Shireen Abu Akleh aliuawa kigaidi kutokana na ukweli kwamba alitumia fursa na jukwa alilopewa na al-Jazeera kufichua njama za kujitanua zinazotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu na wakati huo huo kuanika peupe udhaifu wa utawala huo katika kukabiliana na operesheni za kujitetea zinazofanywa na Wapalestina wanaopigania ukombozi wa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa kibaguzi tangu mwaka 1948.

Kwa kumuua kigaidi na kwa makusudi Shireen Abu Akleh, kwa hakika utawala wa Kizayuni wa Israel ulitaka kulipiza kisasi dhidi ya ufichuaji uliokuwa ukifanywa na mwandishi huyo kuhusiana na ukatili na jinai zinazotekelezwa na Wazayuni katika ardhi za Wapalestina na wakati huo huo kutoa ujumbe wa tahadhari na onyo kwa waandishi wengine ili wasije wakafuata njia iliyofuatwa na mwandishi huyo shujaa katika shughuli zake za upashaji habari huru kuhusu jinai zinazofanywa na Wazayuni katika ardhi hizo.

Kwa maelezo hayo na kwa mujibu wa ushahidi uliopo, Abu Akleh alilengwa kwa makusudi na kuuawa hata kabla ya kuanza operesheni ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo la Jenin na kabla ya yeye na waandishi wenzake kumiminiwa risasi 16, hapakuwa pamesikika milio mingine yoyote ya risasi katika eneo hilo. Tathmini nyingine zilizotolewa kuhusu tukio hilo zinathibitisha wazi kwamba risasi zilizofyatuliwa kuelekea upande aliokuwa Abu Akleh zilikusudiwa kumuua mara moja kwa kuzingatia kuwa alikuwa amevalia kizibao cha kuzuia risasi, hivyo alifyatuliwa risasi sehemu ya mwili iliyokusudiwa kumuua.

Kama alivyokusudia Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, kuwanyamazisha wapinzani wake kupitia mauaji ya kinyama ya Jamal Khashoggi, ili wazije wakamzuia kufikia lengo lake la kuketi kwenye kiti hicho, utawala haramu wa Israel pia ulimuua kikatili Shireen Abu Akleh ili kutia hofu na kujaribu kuwazuia waandishi wengine wa habari kutangaza na kufichua masuala ya Palestina na siasa za kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina, hasa katika eneo la Quds Tukufu na Msikiti Mtakatifu wa al-Aqsa.

Shireen Abu Akleh baada ya kuuawa na Wazayuni akiwa kazini

Kama ilivyofanya serikali ya Joe Biden ambapo imepuuza ahadi zote ilizotoa katika kampeni za uchaguzi, kwa kudai kuwa ingefuatilia faili la mauaji ya Khashoggi, mara hii pia imepuuzilia mbali ahadi ya kufuatilia mauaji ya Abu Akleh na kuamua kusalimu amri mbele ya matakwa na propagansa za utawala wa kigaidi wa Israel kuhusu mauaji ya mwandishi habari huyo.

Kwa ujumla ni kuwa msimamo wa viongozi wa nchi za Magharibi wawe ni wa Marekani au Ulaya kuhusiana na mauaji ya Shireen Abu Akleh, umethibitisha kwa mara nyingine kuwa madai yao ya eti kuunga mkono uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari ni maneno matupu yasiyo na maana yoyote. Msimamo huo imeweka wazi ukweli kwamba suala la haki za binadamu huwa na umuhimu kwao pale tu linapokuwa haligongani na siasa na maslahi yao pamoja na ya utawala haramu wa Israel la sivyo, huwa halina umuhimu wowote kwao na linapaswa kuwa muhanga wa tamaa na siasa zao za kimaslahi katika pembe zote za dunia.