Jul 06, 2022 07:38 UTC
  • Boris Johnson
    Boris Johnson

Mawaziri wawili wa serikali ya Uingereza wamejiuzulu na kung'atuka katika serikali ya Boris Johnson.

Waziri wa Fedha wa Uingereza, Rishi Sunak na mwenzake wa afya Sajid Javid walijiuzulu nyadhifa zao jana Jumanne.

Mawaziri hao wamesema kuwa hawako tayari kuendeleza ushirikiano wao na serikali ambayo inahusika katika migogoro na kashfa.

Ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa serikali ya Boris Johnson, ambayo imekuwa ikikabiliwa na migogoro na kashfa za mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni, sasa inapigania kubakia madarakani kutokana na dharuba zinazoyumbisha utawala wa mwanasiasa huyo.

Kujiuzulu kwa mawaziri hao wawili kumefuatia hatua ya Boris Johnson ya kuomba radhi kutokana na jinsi alivyoshughulikia suala la kujiuzulu kwa naibu mkuu wa chama chake katika Bunge la Uingereza, Chris Pincher.

Waziri Mkuu wa Uingereza alimpandisha cheo Chris Pincher licha ya kufahamu madai ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya mwanachama huyo mkuu wa Chama cha Conservative. 

Pincher alilazimika kujiuzulu baada ya kufichuliwa kwamba amehusika na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wageni wawili wa kike.