Jul 07, 2022 03:33 UTC
  • Marekani yatangaza vikwazo vipya dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran

Wizara ya Fedha ya Marekani imeendeleza uraibu wa nchi hiyo wa kuziwekea vikwazo nchi mbalimbali kwa kutangaza vikwazo vipya dhidi ya sekta ya mafuta na petrokemikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wizara ya Hazina ya Marekani jana Jumatano ilitangaza kuziwekea vikwazo kampuni mbalimbali zenye makao yao katika Umoja wa Falme za Kiarabu, eti kwa kufanikisha mauzo ya bidhaa za mafuta na petrokemikali za Iran zenye thamani ya mamilioni ya dola, katika soko la Mashariki ya Asia.

Wadadisi wa mambo wanasema vikwazo hivyo vinadhihirisha wazi namna Rais Joe Biden wa Marekani ameshindwa kuachana na sera zilizogonga mwamba za mtangulizi wake Donald Trump, za eti mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya taifa la Iran.

Marekani inatumia mjeledi wa vikwazo ili kuiadhibu Iran na kuishinikiza isalimu amri mbele ya matakwa ya Washington, katika mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuiondolea Tehran vikwazo haramu.

Mwezi uliopita pia, Wizara ya Hazina ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya sekta ya petrokemikali ya Iran, na vilevile dhidi ya kampuni za China, Imarati na India zinazotuhumiwa kufanikisha kuuzwa mafuta ya Iran nje ya nchi.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, vikwazo haramu na vya kidhalimu vya Marekani katu havitaizuia Jamhuri ya Kiislamu kuendelea na shughuli zake za kila siku na miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani.

Tags