Jul 07, 2022 07:52 UTC
  • UN: Watu bilioni 2.3 walikumbwa na uhaba wa chakula 2021

Taasisi za Umoja wa Mataifa zimeonya kuwa, kupanda kwa bei za chakula, fueli na mbolea kote duniani kulikosababishwa na vita vya Ukraine kunaiweka dunia katika hatari ya kutumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa chakula na baa la njaa.

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa likiwemo Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Afya Duniani (WHO) yamesema kwa ujumla watu bilioni 2.3 walishuhudia uhaba wa chakula kwa kiwango cha juu na cha wastani mwaka uliopita 2021.

Yamesema katika taarifa ya jana Jumatano kuwa: Watu milioni 828 (karibu asilimia 10 ya jamii ya watu wote duniani) mwaka jana 2021, waliathiriwa na njaa, likiwa ni ongezeko la milioni 46 ikilinganishwa na mwaka juzi 2020, na milioni 150 mwaka 2019.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, idadi ya watu wanaokumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula kwa kiwango cha juu zaidi iliongezeka hadi milioni 924 mwaka jana.

Mashirika hayo ya UN yamesema kupanda kwa bei ya mbolea na nishati mwaka uliopita, imeathiri sekta ya kilimo na hususan mavuno ya ngano, mchele na mahindi. Hali hiyo inahofiwa kuathiri mabilioni ya watu kote Asia, Afrika na Amerika.

Ubaha wa chakula Yemen

Licha ya Wamagharibi kuilaumu Moscow kwa mgogoro wa chakula unaoshuhudiwa duniani, lakini hivi karibuni Rais Vladimir Putin wa Russia alisema ukoloni mamboleo ndio umesababisha migogoro wa kibinadamu inayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali duniani; na kwamba Marekani na nchi za Ulaya ndizo zinazopaswa kubebeshwa dhima iwapo dunia itatumbukia kwenye baa la njaa. 

Alisema usimamizi mbaya wa Wamagharibi kwa uchumi wa dunia na kuyanyonya mataifa dhaifu ndiyo sababu kuu ya kushuhudiwa mfumuko wa bei za bidhaa na mgogoro wa chakula duniani.

Tags