Jul 07, 2022 07:56 UTC
  • Russia yaharibu mifumo ya makombora ya Marekani nchini Ukraine

Jeshi la Russia limetangaza habari ya kusambaratisha mifumo miwili ya makombora aina ya HIMARS ya Marekani mashariki mwa Ukraine.

Wizara ya Ulinzi wa Russia imesema vikosi vya nchi hiyo jana Jumatano vilifanikiwa kuharibu mifumo hiyo miwili ya makombora ya kisasa karibu na medani ya vita katika kijiji kimoja kilichoko katika mji wa Kramatorsk, eneo la Donetsk.

Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema: Karibu na kijiji cha Malotaranovi katika Jamhuri ya Watu wa Donetsk, mifumo miwili ya makombora ya HIMARS iliyotengenezewa Marekani imesambaratishwa na makombora ya Russia yanayopiga shabaha kwa usahihi mkubwa.

Aidha amesema kituo cha rada ya mfumo wa makombora wa S-300 cha Ukraine kimeharibiwa pia, mbali na ngome za mamluki wa kigeni katika mji wa Limany jimboni Mykolaiv.

Vita Ukraine

Mwezi uliopita pia, wanajeshi wa Russia waliteketeza ghala kubwa la silaha za Marekani na Ulaya katika mkoa wa Ternopil wa magharibi mwa Ukraine kwa kutumia makombora ya cruise.

Mara kwa mara Rais Vladimir Putin wa Russia ameonya kuwa, Moscow itaendelea kushambulia silaha zozote za Ukraine hususan zile ambazo nchi za Magharibi zinaipa nchi hiyo.

 

Tags