Jul 07, 2022 15:06 UTC
  • Boris Johnson
    Boris Johnson

Hatimaye Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amejiuzulu uongozi wa Chama cha Conservative baada ya wimbi la kujiuzulu na kung'atuka makumi ya mawaziri wa serikali yake na wanachama wa Chama cha Conservative.

Boris Johnson ametangaza kujiuzulu uongozi wa Chama cha Conservative katika hotuba aliyoitoa leo mbele ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kusema ataendelea kuongoza serikali hadi chama kitakapomteu kiongozi wake mpya. 

Ripoti zinasema Johnson amelazimika kung'atuka baada ya kujiuzulu mawaziri na manaibu waziri zaidi ya 55 wa serikali yake katika muda usiozidi masaa 48. 

Kwa kuzingatia kuwa Chama cha Conservative kina viti vingi katika Bunge la Uingereza, kiongozi mpya wa chama hicho ndiye atakuwa Waziri Mkuu.

Miongoni mwa waliomuacha mkono Boris Johnson na kubwaga manyanga ni aliyekuwa waziri wa elimu, Michelle Donelan ambaye ameachia ngazi chini ya masaa 48 tu baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo. 

Boris Johnson

Serikali ya Uingereza, chini ya uongozi wa Boris Johnson, imekumbwa na madhoruba makali ikiwa ni pamoja na kashfa kadhaa za kisiasa na kijamii kama ile ya Partygate na jinsi alivyoshughulikia suala la kujiuzulu kwa naibu mkuu wa chama chake katika Bunge la Uingereza, Chris Pincher.

Waziri Mkuu huyo wa Uingereza alimpandisha cheo Chris Pincher badala ya kumfuta kazi licha ya kufahamu madai ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya mwanachama huyo mkuu wa Chama cha Conservative. 

Pincher alilazimika kujiuzulu baada ya kufichuliwa kwamba amehusika na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wageni wawili wa kike.