Jul 08, 2022 10:09 UTC
  • Dunia yalaani mauaji ya kigaidi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Japan

Jamii ya kimataifa imeendelea kulaani mauaji ya kigaidi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe.

Zhao Lijian, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema nchi hiyo imepokea kwa mshtuko mkubwa habari za mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe.

Amesema Abe alikuwa rafiki wa China na hivyo nchi hiyo inatoa mkono wa pole kwa familia, serikali na taifa la Japan kwa ujumla kufuatia mauaji hayo.

Naye Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amesema wameshtushwa na kitendo cha kiwoga cha kushambuliwa kwa risasi Shinzo Abe, wakati akitekeleza wajibu wake wa kidemokrasia.

Shinzo Abe aliyekuwa na umri wa miaka 67amepigwa risasi mapema leo Ijumaa alipokuwa akitoa hotuba katika mji wa magharibi mwa Japan wa Nara na kupelekwa hospitalini huku akivuja damu kwa wingi. Mtu mmoja anayeaminika kuwa ndiye aliyempiga risasi Abe ametiwa mbaroni.

Abe alipoteza fahamu na kupata mshtuko wa moyo baada ya kupigwa risasi mbili

Balozi wa Russia nchini Japan, Mikhail Galuzin amesema Moscow inalaani kwa maneno makali kitendo hicho cha kinyama, na kwamba wananchi wa Russia wako pamoja na Wajapan katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Mapema leo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amesema: "Kama nchi iliyoathiriwa na ugaidi na ambayo imepoteza viongozi wakubwa katika hujuma za magaidi, tunafuatilia habari za jaribio la mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe kwa karibu na kwa wasiwasi."

Tags