Jul 12, 2022 07:26 UTC
  • Watu wasiopungua 150 waaga dunia kutokana na mafuriko nchini Pakistan

Watu wasiopungua 150 wamefariki dunia nchini Pakistan kutokana na mafuriko na matukio yanayohusiana na mvua kali zilizonyesha hivi karibuni.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kutoka Islamabad kuwa, maafisa wa kitengo cha masuala la dharura wametoa ripoti usiku wa kuamkia leo kuhusu maafa na hasara zilizosababishwa na mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo hivi karibuni na kutangaza kuwa mji wa Karachi ulioko kusini mwa nchi umekumbwa na mvua kali zaidi za msimu na hasara zilizosababishwa na mvua hizo.

Ripoti hiyo imeeleza pia kuwa, mvua zilizonyesha Baluchistan, ambao ni mkoa unaopakana na ule wa Sistan na Baluchistan wa Iran zimevunja rekodi ya miaka 30 iliyopita, ambapo katika muda wa siku nane zilizopita watu wasiopungua 56 wamefariki dunia katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Baluchistan na kwamba katika maeneo mengine ya Pakistan mvua kali na mafuriko yamesababisha maafa ya roho za watu pia.

Shahbaz Sharif

Sardar Sarafraz, mtaalamu wa mamlaka ya hali ya hewa ya Palestina ametabiri kuwa mvua kali zilizoanza kunyesha siku ya Alkhamisi katika eneo la Karachi zitaendelea kwa muda wa siku kadhaa zijazo.

Katika upande mwingine, Waziri Mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif amemtaarifu Morad Ali Shah, waziri kiongozi wa eneo hilo utayarifu wa serikali kuu kutoa msaada kwa mkoa huo.

Wakati huohuo ripoti zinasema, Jeshi la wanamaji la Pakistan linaendelea na operesheni za utoaji misaada kwa waathirika wa mafuriko sambamba na kuwahamisha watu wanaoishi kwenye maeneo hatarishi zaidi.

Mwaka uliopita pia, mamia ya watu walifariki na kujeruhiwa na nyumba nyingi zilibomoka kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kali za msimu zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Pakistan.../

Tags