Jul 12, 2022 10:06 UTC
  • Ushindi wa chama tawala cha Liberal Democratic Party of Japan katika uchaguzi wa Seneti

Chama tawala nchini Japan cha Liberal Democratic (LDP) na washirika wake wa muungano wa Chama cha Komeito waliimarisha udhibiti wao katikia Baraza la Juu la Bunge la nchi hiyo kwa kushinda zaidi ya viti 75 kati ya viti 125 vya taasisi hiyo.

Uchaguzi huo ulifanyika Jumapili, ikiwa ni siku mbili baada ya kuuawa kigaidi Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe ambaye alikuwa mmoja wa viongozi muhimu katika chama tawala cha LDP. Alipigwa risasi alipokuwa akihutubu katika makutano wa kampeni mjini Nara na kisha akafariki alipokuwa akipata matibabu hospitalini.

Chaguzi za Seneti ya Japan hufanyika kila baada ya miaka mitatu ili kubaini wajumbe 125, ambao ni karibu nusu ya wawakilishi wote 248 wa bunge hilo. Kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya usalama ya eneo lililoathiriwa na mzozo wa Ukraine na umuhimu ambao watu wa Japan wanalipa suala la  usalama wa nchi yao, tunaweza kusema kuwa ushindi mkubwa wa chama tawala cha LDP umetokana na utekelezaji wa mipango ya chama hicho hasa katika masuala ya kijeshi na kiusalama.

Shinzo Abe ambaye alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Japan mwaka 2012 alianza juhudi zake za kuunda jeshi lenye nguvu la Japan na kuondoa nchi yake katika udhibiti wa Marekani katika masuala ya usalama.

Shinzo Abe

Ili kufikia lengo hilo, alihitaji kubadilisha katiba na hasa kifungu cha 9 cha katiba hiyo lakini pamoja na hayo katika muongo mmoja uliopita hakuweza kuimarisha nafasi ya chama cha LDP katika seneti ili kurekebisha katiba.

Hata hivyo, Abe alijitahidi sana kushinda wingi wa viti katika Seneti na ndio sababu alijitokeza katika kampeni za uchaguzi ili chama chake kipate ushindi mkubwa na akiwa katika mkakati huo alipoteza maisha yake. James Brady, mtaalamu wa masuala ya Japan, anasema: "Matamshi ya huruma ya watu wa Japan baada ya kuuawa kwa Abe yalikuwa na athari katika ushindi madhubuti wa chama cha Liberal Democratic na kukiwezesha kuimarisha usalama wa ndani kupitia utekelezaji wa mipango ya Abe, haswa kuhusu kuundwa jeshi lenye nguvu." Moja ya mipango ambayo Shinzo Abe aliifuata ni kuimarisha moyo wa utaifa nchini Japan, unaojulikana kama Shinto, ambao wakati wa utawala wa kifalme wa Meiji uliifanya nchi hiyo kuwa nchi yenye nguvu ya kwanza katika eneo hilo na kuanza kujitanua kuelekea upande wa China na Korea.

Kutokana na hofu ya kurudi katika enzi hizo, baadhi ya watu wa Japan hawakuonyesha hamu kubwa ya kurekebisha katiba, na Shinzo Abe hakuweza kufikia ndoto yake ya kuwa na jeshi lenye nguvu na kuongeza nafasi ya kisiasa na kijeshi ya nchi yake.

Ni kwa sababu hii ndio Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida, akatangaza kuwa amejitolea kutekeleza mipango aliyokuwanayo Abe.

Wananchi wa Japan wakiandamana kupinga uwepo wa vituo vya kijeshi vya Marekani nchini humo

Amin Farjad, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema: "Wazo la Abe lilikuwa uhuru na kuondoea utegemezi ulioko kwa Marekani katika masuala ya usalama. Kimsingi alitaka Japan ijidhaminie usalama wake kama nchi huru. Ni kwa sababu hii, ndio alipata umashuhuru kama mwanasiasa mwenye misimamo ya utaifa wenye misingi ya nguvu ya kitaifa." Kwa vyovyote vile, chama tawala cha Japan cha Liberal Democratic kimepata fursa kubwa ya kupita kutoka hatua ya utegemezi wa kiusalama hadi kufikia hatua ya kuwa na jeshi imara kwa kufanya marekebisho ya katiba, ambayo yakitekelezwa, yatabadilisha hali ya kisiasa na kiusalama ya Japan kwa ujumla.

Muelekeo huo unaoibuka Japan kwa miaka kadhaa sasa umezitia wasiwasi nchi za eneo hilo, haswa China na Korea Kusini.

Tags