Jul 12, 2022 11:05 UTC
  • UN yakaa kimya kuhusu chanzo cha maafa ya kibinadamu Afghanistan

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ukitahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Afghanistan na bila ya kuashiria waliosababisha hali hiyo ya sasa inayowakabili watu wa nchi hiyo iliyoathiriwa na vita umetangaza kuwa, wananchi wa Afghanistan eti wanahitaji misaada ya kibinadamu zaidi.

Miongo miwili ya Afghanistan kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Marekani na pia vita vya ndani vimeharibu na kusambaratisha kwa kiasi kikubwa miundomsingi ya nchi hiyo. Serikali ya muda inayoongozwa na kundi la Taliban ambayo ilishika hatamu za kuiongoza nchi tangu Agosti 15 mwaka jana inahitaji fedha za kutosha ili kuendesha viwanda na uchumi wa Afghanistan. Hata hivyo Marekani mbali na kusitisha au kupunguza misaada iliyokusanywa kwa ajili ya Afghanistan imezuia pia karibu dola bilioni kumi fedha za Waafghani  huku ikitwaa sehemu ya fedha hizo kwa maslahi ya wahanga wa matukio ya Septemba 11.  

Umoja wa Mataifa umesema katika ripoti hiyo kwamba, unafuatilia suala la kuzipatia familia za Waafghani misaada ya haraka ambazo zimekuwa wakimbizi kwa sababu mbalimbali. UN aidha imetahadharisha kuwa, raia na wakimbizi wa ndani ya Afghanistan wanakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na wanahitaji pia misaada ya haraka. 

Filippo Grandi Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi amezitolea wito nchi na taasisi mbalimbali za masuala ya kibinadamu duniani kutoa misaada kwa wananchi wa Afghanistan na kuzitaka kuwa bega kwa bega na raia hao. Afghanistan katika miezi ya karibuni imekumbwa na milipuko ya mabomu na mashambulizi ya kigaidi ya mtawalia yaliyoua mamia ya watu na kuwajeruhi wengine wengi.   

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa UNHCR 

 

Tags