Jul 17, 2022 03:55 UTC
  • Kuendelea mpambano wa Magharibi mkabala wa Russia; mara hii vikwazo vya dhahabu

Nchi za Magharibi zinaendelea kustafidi na wenzo wa mashinikizo kwa Russia kupitia njia mbalimbali kama kuiwekea nchi hiyo vifurushi vya vikwazo vipya kufuatia hatua yake ya kuanzisha vita dhidi ya Ukraine; ambapo Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa uuzaji nje wa dhahabu kutoka Russia utajumuishwa katika kalibu ya vikwazo vipya vya umoja huo.

Tangu kuanza vita kati ya Russia na Ukraine, nchi za Magharibi zimeungana na Marekani katika kuipatia Ukraine misaada mbalimbali; na katika uwanja huo nchi hizo zimeliweka katika ajenda yao ya kazi suala la kuiwekea Russia mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi kupitia njia mbalimbali kama hii ya vikwazo na katika upande wa pili kuiunga mkono na  kuipatia Ukraine misaada ya kijeshi, kilojistiki na kuidhaminia nchi hiyo bajeti kubwa. 

Umoja wa Ulaya hadi sasa umepasisha vifurushi 6 vya vikwazo dhidi ya Moscow; ambapo vikwazo vya karibuni kabisa ni pale nchi wanachama wa umoja huo zilipoamua kusitisha ununuaji mafuta kutoka Moscow kwa kiwango cha asilimia 90 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2022. Umoja wa Ulaya hivi sasa pia umezungumzia kuiwekea Russia vikwazo katika biashara ya dhahabu; ambapo hatua hizo dhidi ya Moscow zimepelekea hali ya uchumi kudhoofika zaidi, kuwepo uhaba wa mafuta na kuongezeka bei ya bidhaa katika nchi za Ulaya kiasi kwamba kupungua mauzo ya gesi ya Russia barani Ulaya kumewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa bara hilo kuhusu kujidhaminia nishati ya mafuta katika msimu wa baridi kali.  

Viktor Orban Waziri Mkuu wa Hungary amevitaja vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Moscow kuwa ni makosa; na kuutolea wito umoja huo kuiondolea Russia vikwazo hivyo. Amesema: Umoja wa Ulaya umeiwekea Russia vifurushi kadhaa vya vikwazo vikali  tangu kuanza vita huko Ukraine. "Vikwazo hivi vimekuwa na taathira kubwa kwa nchi za Ulaya vikiathiri pia sekta ya nishati. Ni wazi kuwa vikwazo vya Ulaya dhidi ya Russia ni sawa na kujimiminia risasi wenyewe Umoja wa Ulaya."    

Viktor Orban, Waziri Mkuu wa Hungary  

Kufeli siasa za vikwazo za Umoja wa Ulaya kumedhihirika wazi zaidi hivi sasa kwa kadiri kwamba si tu nchi nchi za Ulaya pekee ambazo zinapitia hali ngumu ya kiuchumi, bali hata mapato ya Russia pia yameongezeka licha ya hatua hizo za uhasama za Marekani na waitifaki wake. Katika ripoti yake mpya Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA) umetangaza kuwa uuzaji nje mafuta ya Russia mwezi Juni mwaka huu umeongezeka na kufikia zaidi ya dola bilioni 20 licha ya nchi hiyo kutuma shehena ndogo nje ya nchi kutokana na kupanda kwa bei ya nishati duniani.  

Pamoja na hayo, Ulaya katika hatua yake mpya inatarajia kupasisha kifushi kingine cha vikwazo dhidi ya Moscow;  na mara hii imejumuisha pia madini ya dhahabu katika orodha yake hiyo. Russia inazalisha asilimia 8.5 ya dhahabu duniani; na baada ya China na Australia ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa dhahabu duniani ambapo mauzo ya dhahabu ya Russia kimataifa mwaka jana wa 2021 yalikadiriwa kuwa karibu dola bilioni 15. Huko nyuma Marekani, Japan na Canada zilipiga marufuku kuingizwa katika nchi hizo madini ya dhahabu kutoka Russia, na sasa viongozi wa Ulaya wanafanya kila wawezalo ili kujiunga na kambi ya nchi hizo. Wanasema kuwa lengo la marufuku hiyo ni kufunga maficho ambayo hutumiwa na baadhi kukwepwa vikwazo vya zamani dhidi ya Moscow.  

"Marosh Shefchovich Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulaya amedai kuhusiana na hilo kuwa umoja huo kwa kushadidisha vikwazo dhidi ya Russia unataka  kusaidia kuhitimisha vita huko Ukraine haraka iwezekanavyo. 

Marosh Shefchovich, Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulaya 

Rais Joe Biden wa Marekani ndiye aliyezungumzia kwa mara ya kwanza suala la kuiwekea Russia vikwazo vya dhahabu eti kama njia ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Moscow, hata hivyo nchi zote wanachama wa EU zinapasa kuafiki mpango huo licha ya kuungwa mkono na baadhi tu ya nchi za Ulaya kama alivyotangaza Kansela wa Ujerumani kwamba pendekezo la Marekani kwa Umoja wa Ulaya la kuiwekea Russia vikwazo vya kuuza nje dhahabu yake linapasa kujadiliwa ndani ya umoja huo. Kamisheni ya Ulaya aidha inatazamia kuchunguza vikwazo vya dhahabu dhidi ya Russia katika siku zijazo. 

Hii ni katika hali ambayo inaonekana kuwa katika mazingira ya sasa marufuku hiyo ya dhahabu dhidi ya Russia huenda zaidi ikawa ni hatua ya kimaonyesho tu kwa sababu vikwazo vya nchi za Magharibi kwa kiasi kikubwa vimepelekea kufungwa masoko ya Ulaya na Marekani kwa dhahabu ya Russia. Hasa ikizingatiwa kuwa, kuna uwezekano vikwazo vya dhahabu dhidi ya Russia pia vikawa na taathira chanya sawa kabisa na kile kilichotokea katika kadhia ya vikwazo vya mafuta na gesi dhidi ya nchi hiyo.

 

Tags