Jul 21, 2022 04:29 UTC
  • Kutuhumiwa India kuwa inaunga mkono makundi ya magaidi yaliyoko Afghanistan

Balozi wa Pakistan mjini Kabul amesema, India inayaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Afghanistan ili kuvuruga amani na usalama ndani ya Pakistan.

Mansour Ahmad Khan amedai kuwa, kwa muda wa miongo miwili sasa, serikali ya India imekuwa ikiyaunga mkono makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao nchini Afghanistan kwa lengo la kuvuruga usalama ndani ya Pakistan na hata imekuwa ikiyapatia mafunzo na kuyafadhili kifedha pia makundi hayo.

Ahmad Khan ameendelea kueleza kwamba, India imekuwa na nafasi haribifu Afghanistan na akafafanua kuwa, katika miongo kadhaa iliyopita, New Delhi imekuwa na nafasi haribifu kwa kutekeleza na kuendesha harakati za kigaidi ndani ya Pakistan kupitia Afghanistan.

Mansour Ahmad Khan

Pamoja na hayo, balozi wa Pakistan mjini Kabul amesema, "serikali ya Taliban imetoa hakikisho kuwa ardhi ya Afghanistan haitatumika dhidi ya nchi nyingine yoyote ikiwemo Pakistan; na sisi tunakaribisha ahadi hii."

Kutuhumiwa India kuwa inawaunga mkono magaidi walioko Afghanistan dhidi ya Pakistan ni mwendelezo wa sera ambazo Islamabad imekuwa ikizifuata kwa angalau miongo miwili sasa kuhusiana na New Delhi. Pamoja na hayo tuhuma za kuunga mkono ugaidi ni mwenendo wa pande zote mbili, kwa sababu katika miaka ya karibuni kila moja kati ya India na Pakistan imekuwa ikimtuhumu mwenzake kuhusika na suala hilo.

Kwa mtazamo wa serikali ya Pakistan, India inayaunga mkono makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao ndani ya ardhi ya Afghanistan yakiwemo ya Tehrik Taliban Afghanistan na DAESH (ISIS) kwa lengo la kudhoofisha usalama wa Pakistan na kwamba miongoni mwa nyenzo inazotumia ni kuyasaidia kifedha makundi hayo. 

Kwa kuzingatia kuwa msimamo wa Taliban wa kukazania kutumia nguvu na uwezo wake tu kwa ajili ya kuendesha nchi na kukataa kuunda serikali pana na shirikishi umevuruga mno hali ya kisiasa na kiusalama ya Afghanistan, suala hilo limetoa fursa zaidi kwa makundi ya kigaidi kushamirisha harakati zao nchini humo.

Ukiwa umepita takriban mwaka mmoja sasa tangu Taliban itwae tena madaraka ya nchi, kundi la kigaidi la Daesh limefanya mashambulio kadhaa katika maeneo tofauti ya Afghanistan ukiwemo mji mkuu Kabul ulio na hali afadhali zaidi kiusalama kulinganisha na miji mingine ya nchi hiyo; jambo ambalo limezusha malalamiko mengi ya makundi mbalimbali ya watu kuhusiana na utendaji wa serikali ya Taliban katika masuala ya usalama.

Matamshi ya balozi wa Pakistan mjini Kabul yanaonyesha kuwa, Islamabad, nayo pia imekasirishwa na hali isiyoridhisha ya kiusalama inayotawala hivi sasa nchini Afghanistan, ambayo inaandaa mazingira mwafaka ya kuyashimirisha harakati za magaidi na inahisi kuwa, mazingira kama hayo yanaipatia India fursa nzuri ya kuwaunga mkono watu wenye misimamo ya kufurutu ada kwa ajili ya kuvuruga na kuhatarisha usalama wa ndani ya Pakistan.

Lakini kama tulivyotangulia kueleza, tuhuma za kuunga mkono ugaidi, ni suala ambalo hata India pia imelitumia mara kadhaa dhidi ya Pakistan na hata ikafika mbali zaidi kwa kuzitaka taasisi za kimataifa na washirika wake wa Magharibi waishinikize Islamabad ili iache kuunga mkono makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Magaidi wa kundi la DAESH (ISIS)

Viongozi wa Pakistan wanahofu kwamba, India inaweza kutumia wenzo wa upelekaji misaada ya kibinadamu huko Afghanistan wakati huu wa utawala wa Taliban ili izidi kuwa na ushawishi ndani ya kundi hilo. Jambo hilo, wanahisi litapanua wigo wa uwepo wa India ndani ya nchi hiyo na kwa mtazamo wa Islamabad ni tishio na hatari kwa usalama wa Pakistan.

Nukta yenye kutoa mguso hapa ni kwamba, hivi sasa India inatuhumiwa kuwa inawaunga mkono magaidi walioko ndani ya ardhi ya Afghanistan kwa lengo la kuvuruga usalama wa taifa wa Pakistan ilhali katika miezi ya hivi karibuni maafisa wa Islamabad wamekuwa wakitoa miito ya kuanzishwa tena mazungumzo ya kutafuta suluhu na amani kati ya nchi mbili.../

 

 

Tags