Jul 26, 2022 11:18 UTC
  • Pakistan: Kauli ya waziri wa ulinzi wa India kuhusu Kashmir ni ya kichochezi

Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imesema kauli aliyotoa waziri wa ulinzi wa India, kwamba eneo la Kashmir ni milki ya nchi hiyo ni ya kichochezi.

Kwa mujibu wa chaneli ya televisheni ya NDTV ya India, waziri wa ulinzi wa India Rajnath Singh, ambaye jana Jumatatu alitembelea eneo la Jamu na Kashmir alidai kwamba, Kashmir iliyo chini ya mamlaka ya Pakistan nayo pia ilikuwa na itabaki kuwa sehemu ya ardhi ya India.

Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imetoa taarifa kujibu matamshi ya Singh kwamba "Kashmir iliyo chini ya mamlaka ya Pakistan nayo pia ni milki ya India" ikisisitiza kuwa kauli hiyo ni ya "kichochezi na haikubaliki hata kidogo".

Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imesisitiza katika taarifa yake hiyo kwamba, waziri wa ulinzi wa India amepotosha ukweli wa kihistoria kuhusu mzozo wa Jamu na Kashmir na kutoa vitisho na madai yasiyo na msingi dhidi ya Islamabad.

Pakistan na India zimeshawahi kupigana vita kwa sababu ya mzozo wa Kashmir

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imeeleza kuwa, Islamabad inaunga mkono kupatikana suluhu na uthabiti katika eneo lakini ikaonya pia kwamba, Pakistan inao uwezo wa kukabiliana na mpango wowote wa hujuma dhidi yake.

Kashmir ni moja ya masuala muhimu zaidi yanayozozaniwa na India na Pakistan ambapo kila nchi inadai haki ya umiliki wa eneo hilo.

Wakashmir wa eneo linalodhibitiwa na India wanataka litekelezwe azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloagiza kuitishwa kura ya maoni ya kuamua hali na hatima ya eneo hilo, lakini serikali ya New Delhi inapinga kutekelezwa azimio hilo.../

Tags