Jul 27, 2022 06:14 UTC
  • Kanisa Katoliki laomba msamaha kuhusu mauaji ya Kimbari ya Wacanada asilia

Hatimaye, baada ya kusubiri kwa muda mrefu, Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki, amekwenda Canada na kuomba msamaha kwa wenyeji asilia wa nchi hiyo kutokana na kuhusika kanisa hilo katika moja ya jinai na maafa mabaya zaidi ya kibinadamu nchini humo.

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, kugunduliwa makaburi ya halaiki na miili ya mamia ya watoto nchini Canada kumeibua suala la mauaji yaliyofanywa dhidi ya wenyeji na ubaguzi wa rangi dhidi yao. Ukubwa wa janga hilo la kibinadamu uliwapelekea wanaharakati wa mashirika ya kiraia ya Canada na viongozi wa kisiasa nje ya mipaka ya Canada kulalamikia vikali suala hilo kiasi kwamba Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, alilazimika kukosoa uzembe uliofanywa na serikali ya nchi hiyo na pia kulibebesha Kanisa Katoliki dhima ya maangamizi hayo ya umati na wakati huo huo kumtaka Papa wa kanisa hilo asafiri nchini humo ili kuwaomba msamaha jamaa na familia za wahanga wa mauaji hayo.

Kwa miongo kadhaa, Kanisa Katoliki la Canada na kwa msaada na ushirikiano wa serikali, lilikuwa likiwatenganisha kwa nguvu watoto asilia wa nchi hiyo na familia zao na kisha kuwapeleka katika shule za bweni. Shule hizo ziliendeshwa na makanisa kuanzia miaka ya 1840 hadi 1990. Hatua hiyo isiyo ya kibinadamu ilichukuliwa kwa madai ya kuwaunganisha kijamii na raia weupe wa Canada.

Papa Francis akiwa na viongozi wa makabila asilia ya Canada

Watoto hao walikabiliwa zaidi na unyanyasaji, ubakaji na utapiamlo katika vituo hivyo vya bweni, hivi kwamba wengi wao hawakuweza kustahimili hali hiyo ngumu na hatimaye kupoteza maisha. Wengi wao pia waliuawa kwa sababu mbalimbali. Isitoshe, si serikali wala shule zilichukua jukumu la kusajili majina ya wanafunzi waliofariki bali hata hazikuchukua hatua yoyote ya kuzifahamisha familia zao kuhusu vifo vya watoto wao. Wengi wa watoto waliokufa au kuuawa walizikwa katika makaburi ya umati yasiyojulikana.

Mzozo kuhusu maafa yaliyotokea katika shule hizo ulianza mwaka 2021 kwa kugunduliwa mabaki ya watoto 215 katika eneo la shule ya bweni ya Wacanada asilia katika jimbo la British Columbia magharibi mwa nchi. Ukubwa wa maafa hayo ya kibinadamu ulikuwa wa kutisha kiasi kwamba Tume ya Kutafuta "Ukweli na Maridhiano" iliyataja kuwa mauaji ya kimbari ya kitamaduni. Tume hiyo ilisema mfumo wa shule za bweni ulisababisha mauaji ya kitamaduni katika familia za asilia za Kanada ambayo yatabakia kutoka kizazi hadi kizazi.

Katika siku za kwanza za kufichuliwa habari kuhusu mauaji ya kimbari ya watoto wa kiasilia nchini Kanada, wakuu wa Kanisa Katoliki walikataa kuomba msamaha kuhusu hilo. Ingawa Papa Francis alisema katika majibu yake ya kwanza kuhusu maafa hayo kwamba alichukizwa sana na kushtushwa na tukio hilo, lakini jilo halikuweza kuponya maumivu na mateso ya wenyeji wa Kanada.

Kadiri muda ulivyopita na kina cha maafa hayo kudhihirika zaidi, hatimaye Papa Francis alitangaza kwamba alikuwa amesikitishwa na tabia ya “baadhi ya Wakatoliki” na akapanga kuelekea Kanada.

Sasa, baada ya kupita miezi kadhaa ya kusubiri, kiongozi wa Wakatoliki duniani amesafiri Kanada. Wakati wa safari hiyo, ametoa hotuba kwa walionusurika katika jinai ya shule za Kikristo za Kanada na kuwaomba msamaha. Papa Francis ameelezea safari yake hiyo kuwa ni ya "kutubu na kulipa fidia" kutokana na kitendo kilichofanywa na wamishonari wa Kanisa Katoliki katika unyakuzi wa kulazimishwa wa vizazi kadhaa vya watoto wa kiasili wa Kanada.

George Arcand Junior, Mkuu wa Shirikisho la Makabila Sita ya Kwanza ya Kanada, ameelezea matumaini kwamba baada ya Papa kuwaomba msamaha, sasa wataweza kuanza safari yao ya kutafuta uponyaji kutokana na mateso na machungu waliyopitia, na kwamba hali ambayo imekuwepo kwa miaka mingi dhidi ya watu wa asili wa Canada itabadilika.

Sehemu nyingine ya safari ya Papa Francis nchini Canada

Safari ya Papa Francis nchini Kanada na kukiri kudhulumiwa wenyeji asili wa nchi hiyo na ombi lake la msamaha, ingawa ni sehemu ya matakwa ya wenyeji wa nchi hiyo, lakini haipunguzi uhusikaji wa serikali ya Kanada katika jinai hiyo. Kwa hakika haiwezekani kuwa mauaji hayo makubwa ya halaiki ya watoto asilia wa Canada ambayo yalidumu kwa karibu karne moja, yalifanyika bila ufahamu wa viongozi wa serikali ya nchi hiyo. Kwa hiyo, serikali ya Kanada kama lilivyo Kanisa Katoliki, inapasa kulaumiwa na kuwajibishwa kuhusu maafa hayo makubwa ya kibinadamu nchini humo.

 

Tags