Jul 31, 2022 05:04 UTC
  • Safari ya Mohammed bin Salman nchini Ufaransa; haki za binadamu zilizosahaulika

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman aliwasili mjini Paris siku ya Alhamisi Julai 28, na kukaribishwa vizuri na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Jumatano iliyopita, Bin Salman aliingia katika nchi ya Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2018 ambapo waziri mkuu wa Ugiriki alikuwa mwenyeji wake. Alhamisi Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alimkaribisha kwa furaha Mohammed bin Salman mjini Paris. Huo ulikuwa mkutano wa pili kati ya bin Salman na Macron katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja. Rais wa Ufaransa alisafiri hadi Saudi Arabia mnamo Desemba 2021 kwa ajili ya kuzungumza na Mohammed bin Salman. Katika safari yake ya mjini Paris hapo Alhamisi, Bin Salman alienda kwenye kasri lake la kifahari katika viunga vya jiji la Paris, ambalo linasemekana kuwa ni jumba lenye gharama kubwa zaidi duniani.

Wiki mbili zilizopita, safari ya Rais Joe Biden wa Marekani mjini Jeddah ambapo alikutana na kuzungumza na mwanamfalme wa Saudia ulikuwa mwanzo wa safari za Mohammed bin Salman barani Ulaya. Vyombo vya habari vya kimataifa, likiwemo shirika la habari la Reuters, vimezingatia mazungumzo ya Macron na Mohammed bin Salman kama sehemu ya juhudi za nchi za Magharibi kupata uungaji mkono wa Saudi Arabia kama moja ya nchi kuu zinazozalisha mafuta huku vita vya Ukraine vikiendelea.

Bin Salman alihusishwa pakubwa na mauaji ya Jamal Khashoggi

Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya, pamoja na Marekani, zinajaribu kufidia hasara ya nishati iliyopatikana kufuatia shambulio la Russia dhidi ya Ukraine. Baada ya kuishambulia Ukraine, Russia imeacha kutuma gesi barani Ulaya ikiwa ni katika kujibu vikwazo vya nchi za Magharibi na uungaji mkono wao kwa Ukraine. Waziri Mkuu wa Ufaransa amesema kuhusu safari ya Mohammed bin Salman mjini Paris kwamba ilikuwa na lengo la kujadili suala la mafuta.

Mbali na suala la mafuta, hali ya kiuchumi na kijamii ya Ufaransa ni jambo jingine muhimu ambalo limejadiliwa katika safari ya Mohammed bin Salman mjini Paris. Mfumuko wa bei wa zaidi ya asilimia 10 nchini Ufaransa na hofu ya uhaba mkubwa wa mafuta katika msimu wa  baridi kali ni wasiwasi mkubwa unaomkabili rais wa Ufaransa kwa sasa. Mbali na hayo, Ufaransa ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa silaha kwa Saudi Arabia.

Safari ya Bin Salman nchini Ufaransa imekosolewa na duru za haki za binadamu kwa kupuuza nafasi ya Bin Salman katika mauaji ya Jamal Khashoggi mwaka 2018, ukosoaji ambao umefumbiwa macho na viongozi wa Ufaransa ambapo hata polisi wa nchi hiyo wamezuia kufanyika maandamano yoyote dhidi ya Bin Salman.

Yannick Jado, kiongozi wa Chama cha Kijani na mjumbe wa Bunge la Ulaya, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba, hakuna jambo lolote lililojadiliwa katika mazungumzo ya Macron na Mohammed bin Salman kuhusu mwili uliokatwa vipande vipande wa mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi, uchafuzi wa hali ya hewa, amani wala haki za binadamu bali suala lililopewa umuhimu katika mazungumzo hayo ni kuhusu mafuta na silaha! Mambo ambayo hayapaswi kujadiliwa kabisa katika kipindi hiki. Baadhi ya vyombo vya habari pia vilitumia anwani ya "haki za binadamu zilizosahaulika" katika kuelezea makaribisho makubwa aliyopewa Bin Salman na Rais Emmanuel Macron huko Paris.

Emmanuel Macron amempokea Bin Salmn nchini kwake huku akipuuza misingi yote ya haki za binadamu

Suala muhimu ni kwamba safari ya Bin Salman nchini Ufaransa inakamilisha duru mpya ya mchakato wa kupokelewa kwake katika ngazi za kimataifa na hasa katika nchi za Magharibi bila tatizo lolote, na hivyo kuthibitisha wazi madai ya uongo yanayotolewa na nchi hizo kuhusiana na suala zima la eti kutetea haki za binadamu. Agnes Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Kurejeshewa hadhi mwanamfalme huyu muuaji  nchini Ufaransa kama walivyofanya viongozi wa Marekani, kutahalalisha vitendo viovu vya mwanamfalme huyo. Jambo tunaloomba ni kukabiliana na ukweli wa mambo kama ulivyo." Kanali ya France 24 pia imeandika kuhusiana na suala hilo kwamba, safari ya Bin Salman nchini Ufaransa inachukuliwa kuwa hatua ya hivi punde zaidi ya kumpokea mwanamfalme huyo wa Saudi Arabia katika uga wa kimataifa, tukitilia maanani kwamba kabla ya hapo Rais Joe Biden wa Marekani pia alikutana naye mjini Riyadh mapema mwezi huu.

Tags