Aug 01, 2022 16:59 UTC
  • Mahakama ya ICC yashindwa kuchunguza uhalifu wa kivita nchini Afghanistan

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) bado wanasitasita kuhusu suala la kuendeleza uchunguzi wa uhalifu wa kivita uliofanyika nchini Afghanistan.

Kabla ya kundi la Taliban kutwaa tena madarakani nchini Afghanistan mwaka jana, jambo lililozingatiwa zaidi na majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai lilikuwa uchunguzi wa uhalifu wa kivita uliofanywa na vikosi vya majeshi ya kigeni vilivyokuwa Afghanistan, hasa vikosi vya Marekani. Hata hivyo vitisho vilivyotolewa na Marekani hususan serikali ya Donald Trump dhidi ya majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kwamba iwapo mahakama hiyo itachunguza uhalifu wa kivita uliofanywa na majeshi ya Marekani huko Afghanistan, Washington itafuta visa zao za kuingia katika nchi hiyo na kupunguzua mchango wake katika mahakama ya ICC, vimekwamisha uchunguzi wa jinai za kivita uliofanywa na Wamarekani huko Afghanistan. Hii ni licha ya kwamba, uchunguzi uliofanywa na kamati za kutafuta ukweli umethibitisha kuwa wanajeshi wa Marekani wamefanya uhalifu wa kivita nchini Afghanistan.  

Ali Vahidi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema: "Wamarekani walifanya jinai nyingi nchini Afghanistan, kuanzia kuua familia, kutesa, kutia mbaroni watu kinyume cha sheria na kukata miili ya watu hadi kuchoma Qur'ani Tukufu na kuvunjia heshima matukufu ya Waafghani. Hata hivyo uhalifu huo wa kivita haujawahi kushughulikiwa katika mahakama yoyote."

Miongoni mwa sababu zilizoifanya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kushikwa na kigugumizi na kusuasua katika kadhia ya kuchunguza jinai za kivita zilizofanywa na majeshi ya Marekani nchini Afghanistan ni kubadilishwa mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, ambako kuna uwezekano mkubwa kwamba kulifanyika kwa shinikizo la Marekani. Karim Khan, Mwendesha Mashtaka mpya na Mwingereza wa mahakama hiyo, ambaye alianza kazi baada ya Taliban kutwaa tena mamlaka, amewataka majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuchunguza uhalifu unaohusiana na Taliban na kundi la kigaidi la ISIS nchini Afghanistan na si jinai zilizofanywa na majeshi ya nchi za Magharibu hususan Marekani katika nchi hiyo. Karim Khan alidai kuwa uchunguzi wa uhalifu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan haufai tena!

Karim Khan amejisahaulisha kwamba familia nyingi za Waafghani waliopoteza wapendwa wao waliouawa bila ya hatia yoyote na majeshi ya Marekani, zimefungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).  

Mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Soroush Amiri anasema: "Kuwekwa kando uchunguzi wa jinai za kivita zilizofanywa huko Afghanistan kuna maana ya kupuuzwa uhalifu uliofanywa na Marekani kwa watu wa Afghanistan na kwa wanadamu wote. Hii ni kwa sababu Marekani imetenda jinai na uhalifu kama huo mahala popote ilipoweka mguu; hivyo jamii ya kimataifa ilikuwa na matumaini kwamba, sehemu ndogo ya jinai hizo za Marekani zilizofanyika huko Afghanistan ingeshughulikiwa na kuchunguzwa katika mahakama ya ICC." 

Makaburi ya raia wa Afghanistan waliouawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani

Alaa kulli hal, kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan kwa miongo miwili kumeandamana na jinai za kutisha zilizotendwa na majeshi hayo pamoja na vikosi vya jeshi la Uingereza, na hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya kufumbia macho jinai na uhalifu huo haitawafanya walimwengu wasahau jinai hizo au kuwatakasa wahalifu hao. Hii ni pamoja na kuwa hatua hiyo ya mahakama ya ICC inashusha chini hadhi yake mbele ya walimwengu hususan Waafghani ambao walikuwa na matumaini kwamba chombo hicho cha kimataifa cha kushughulikia jinai na uhalifu wa kivita kingewatendea haki katika kadhia hiyo.  

Tags