Aug 05, 2022 10:52 UTC
  • Hujuma za chuki dhidi ya Waislamu Canada zaongezeka kwa 71%

Jinai zinazotokana na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu zimeongezeka kwa kiwango cha kutisha nchini Canada.

Utafiti mpya uliofanywa na Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada  (NCCM) umeonyesha kuwa, hujuma za chuki dhidi ya Waislamu nchini humo ziliongezeka kwa asilimia 71 mwaka uliopita 2021.

Utafiti huo umebaini kuwa, visa vilivyosajiliwa vya kushambuliwa Waislamu kwa misingi ya dini yao iliongezeka kutoka 84 mwaka 2020, hadi 144 mwaka jana wa 2021.

Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada limesema Waislamu kadhaa waliuawa katika hujuma hizo, huku likitoa mfano wa tukio la kuuawa Waislamu wanne wa familia moja wenye asili ya Pakistan mnamo Juni mwaka jana mjini Ontario, baada ya mtu mwenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu kuwagonga na gari kwa makusudi.

Waislamu wliouawa Ontario Juni 2021 kwenye shambulio la kigaidi

Aprili mwaka huu, watu watano walijeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi na wahalifu wasiojulikana wakiwa msikitini nchini Canada, huku vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vikionekana kushtadi nchini humo.

Uislamu ni dini inayoenea kwa kasi zaidi Canada ambapo Waislamu wameongezeka kwa asilimia 82 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Hivi sasa Waislamu ni karibu asilimia 3.5 ya watu wote milioni 38 nchini Canada. Kutokana na hali hiyo kumekuwepo jitihada za makusudi za kueneza chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Waislamu wa Canada hivi sasa wanaishi kwa hofu kutokana na kushtadi visa vya uhalifu na hujuma dhidi yao na matukufu yao. Serikali ya Canada imekuwa ikikosolewa pia kwa kuwawekeka mbinyo Waislamu kupitia sheria zake, kama ya kupiga marufuku vazi la Hijabu katika maeneo ya umma.

Tags