Aug 06, 2022 03:50 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani Ufaransa kwa kupiga marufuku hijabu ya wanawake wa Kiislamu

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa karibuni na Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Ufaransa imekiuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa kwa kumzuia mwanamke mmoja aliyekuwa amevalia hijabu kushiriki kwenye kozi ya elimu ya watu wazima iliyofanyika katika shule moja ya upili nchini humo.

Uamuzi huo wa Kamati ya Haki za Binadamu, ambao ulifanywa mnamo Machi, lakini uliwasilishwa kwa wakili wa mlalamikaji Jumatano iliyopita, ulifuatia malalamiko yaliyowasilishwa mnamo 2016 na mwanamke mmoja raia wa Ufaransa aliyezaliwa mwaka 1977. Wakili wa mlalamikaji aliomba jina la mteja wake lisitajwe. Mnamo 2010, mlalamikaji alihudhuria kozi ya mafunzo ya ufundi kwa watu wazima. Baada ya kukubaliwa katika mahojiano na mtihani wa kuingia shuleni, alikwenda katika Shule ya Upili ya Langevin Wallon ambapo mafunzo yalipaswa kufanyika. Lakini mkuu wa shule hiyo alimzuia kuhudhuria kozi hiyo ya mafunzo kwa sababu ya marufuku iliyokuwepo kuhusu nembo zinazoonyesha mwelekeo wa kidini katika taasisi za elimu za serikali.

Wanawake wa Kiislamu wakitetea vazi lao la hijabu nchini Ufaransa

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema: “Kizuizi kilichowekewa mlalamikaji kwamba haruhusiwi kuhudhuria darasani akiwa amevalia hijabu ni kizuizi kinachokiuka Mkataba wa Kimataifa wa Uhuru wa Kiraia na Kisiasa, unaoathiri uhuru wake wa kuabudu." Kamati hiyo inakumbusha kwamba uhuru wa mtu kudhihirisha dini yake unajumuisha matumizi ya nguo au mtandio maalumu, na kusisitiza kwamba marufuku hiyo ni kizuizi cha wazi cha uhuru wa mtu kudhihirisha dini yake. Sefen Guez Guez wakili wa mlalamikaji katika kesi hiyo anasema: "Huu ni uamuzi muhimu unaoonyesha kwamba Ufaransa inapaswa kufanya juhudi za kurekebisha msimamo wake kuhusu haki za binadamu, hasa katika uwanja wa kuheshimu wafuasi wa dini za waliowachache na hasa jamii ya Waislamu."

Uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya wanawake wa Kiislamu kuvaa hijabu nchini Ufaransa kwa hakika unabatilisha uongo wa madai ya utawala wa Ufaransa kuhusu kuwepo uhuru na haki sawa za raia katika nchi hiyo. Kwa muda mrefu sasa wasichana na wanawake wa Kiislamu nchini Ufaransa ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya wamekuwa wakikabiliwa na mashinikizo na vikwazo vya kila aina kutokana na kuvaa hijabu. Wamekuwa wakiwekewa vikwazo mbalimbali katika uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuwapiga marufuku kusoma kwa sababu tu ya kuvaa hijabu.

Mwenendo huo wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Ufaransa umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Mashinikizo na vikwazo hivyo dhidi ya Waislamu na Uislamu ambavyo vimeongezeka maradufu katika kipindi cha utawala wa Emmanuel Macron, rais wa mrengo wa kati wa Ufaransa na ambavyo vinakwenda sambamba na kupitishwa sheria kali dhidi ya hijabu na vituo vya mafunzo ya Kiislamu vimeyafanya maisha ya Waislamu kuwa magumu katika nchi hiyo.

Mnamo Februari 2022, serikali ya Ufaransa ilitangaza kuunda taasisi mpya iliyopewa jina la "Jumuiya ya Uislamu ya Ufaransa" kwa madai ya kuwafungamanisha Waislamu wa nchi hiyo na utamaduni na jamii ya Ufaransa na kupiga vita misimamo mikali. Kuanzishwa taasisi hiyo ambayo ni sehemu ya juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Emmanuel Macron, ili kudhoofisha Uislamu nchini Ufaransa, kulivunja kivitendo shughuli za taasisi ya awali kama hiyo iliyokuwa ikiitwa "Baraza la Waislamu wa Ufaransa."

Mabinti wa Kiislamu wakitetea viza lao la staha la hijabu

Hatua hizo za Macron zinatokana na fikra ya "usekulari wa kihujuma" ambayo inashajiisha hujuma kali dhidi ya dini na nembo za kidini katika jamii. Kimsingi, Macron hana mtazamo mzuri kuhusu Uislamu, na ameunga mkono kivitendo hatua yoyote inayopinga na kudhoofisha Uislamu pamoja na kumvunjia heshima Mtukufu Mtume (saw). Hatua hizo ni pamoja na kutetea kutusiwa Mtume Mtukufu (saw) kwa kuruhusu kuchapishwa vikatuni vinavyomvunjia heshima, kuwafukuza Waislamu Ufaransa na kufunga misikiti na vituo vyao vya kidini na vilevile kuwasilisha bungeni muswada wa kuimarisha itikadi za usekulari, ambao kimsingi unalenga kuhujumu Uislamu katika Jamii ya Ufaransa. Masoud Shajareh, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu anasema: Macron ameushambulia Uislamu waziwazi na kudai kuwa uko katika mgogoro, katika hali ambayo kwa hakika ni siasa za Ufaransa na wanasiasa wa Ulaya walio na mtazamo kama wake ndio wako kwenye mgogoro.

Tags