Aug 06, 2022 10:45 UTC
  • Mlipuko wa kigaidi mjini Kabul, malengo na matokeo yake

Kundi la kigaidi la Daesh au kwa jina jingine ISIS, limekiri kuhusika na mlipuko uliotokea jana Ijumaa huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, ambao ulipelekea watu 8 kuuawa shahidi na wengine 18 kujeruhiwa.

Tangu takriban mwaka mmoja uliopita tokea kundi la Taliban lirejee madarakani nchini Afghanistan, kundi la kigaidi la Daesh limefanya mashambulizi na milipuko mingi ya kigaidi katika nchi hiyo, ikiwemo milipuko mikubwa ya umwagaji damu iliyotokea katika mikoa ya Kunduz na Balkh. Hii ni licha ya kwamba Taliban daima imekuwa ikidai kuangamiza au kulidhoofisha pakubwa kundi hilo. Kwa kuzingatia hilo, mlipuko wa Ijumaa huko Kabul unaweza kutathmiiwa katika mitazamo miwili.

Mtazamo wa kwanza ni kuwa kundi la kigaidi la Daesh linatunisha misuli na kudhihirisha nguvu zake mkabala wa hatua za kiusalama za Taliban ili kuthibitisha udhaifu wake mbele ya kundi hilo na pili ni kwamba katika kukaribia siku za maombolezo za Tasua na Ashura  ya Imam Hussein (as), ambapo Taliban imechukua hatua kali za kiusalama, mlipuko huo wa kigaidi, unaibua dhana kwamba huo ni utangulizi wa Taliban kutekeleza siasa kali dhidi ya maombolezo ya kuuawa Shahidi Imam Hussein (as) na wafuasi wake wachache waaminifu.

Ali Wahedi, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan, anasema:

Mlipuko wa karibuni mjini Kabul

"Tunapasa kuweka tofauti kati ya fikra na itikadi za Taliban ya Afghanistan na Taliban kutoka nje, ambayo kwa hakika ni ule mtandao wa Haqqani. Tunachokishuhudia sasa kuhusiana na masuala ya kimadhehebu na kiutendaji nchini Afghanistan kimeathiriwa na fikra za mtandao wa Haqqani unaoshirikiana na Daesh, na kwa mujibu wa maneno ya Hamid Karzai, rais wa zamani wa Afghanistan, kundi hilo pia linapata maelekezo kutoka Pakistan.

Taliban wanajua vyema kwamba ili kuendeleza utawala wao na kutambuliwa kimataifa, wanahitaji kuimarisha umoja wa kitaifa na maingiliano chanya na jamii ya kimataifa. Hii ni katika hali ambayo mipango ya Taliban, ikiwa ni pamoja na kufunga shule za wasichana na kufutwa siku rasmi za mapumziko za Ashura na Nowruz katika kalenda ya Afghanistan, inapingana wazi na malego hayo. Kwa kuzingatia historia ya maingiliano ya Taliban wa Afghanistan na jami ya nchi hiyo na pia kuheshimu kwao mila na desturi za madhehebu ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na maombolezo ya Ashura ya Imam Hessein (as),  bila shaka kundi la Taliban ya Haqqani linachukua hatua ambazo zinalenga kuibua mgawanyiko wa kimadhehebu na kijamii nchini humo. Kundi hilo na kwa uungaji mkono wa Pakistan, sio tu limechukua hatua ya kubuni siasa za kijamii na kimadhehebu huko Afghanistan, bali linajaribu kuigeuza nchi hiyo kuwa pango la magaidi.

Abulfazl Zuhrewand, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema:

"Tangu mwanzo, Taliban wa Haqqani kwa kushambulia Kabul na kuchukua madaraka kwa nguvu, walionyesha kuwa wao ni tofauti na Taliban wa Afghanistan ambao waliamua kufanya mazungumzo na Marekani kwa miaka miwili huko Doha, nayo Pakistan kwa kuwatwisha watu wa Afganistan mtandao wa Haqqani, si tu kwamba imewatenga Taliban wa Afghanistan, bali inalenga kuibua mgawanyiko wa kimadhehebu na kijamii nchini humo.

Nembo za maombolezo ya Muharram katika moja ya misikiti ya Kabul

Kwa vyovyote vile na kwa kutilia maanani uwezekano mkubwa wa kuwepo uhusiano kati ya mtandao wa Haqqani na Daesh pamoja na makundi mengine ya kigaidi ambayo yana majina na anwani tofauti, tunaweza kusema kwamba mlipuko wa Ijumaa huko Kabul ulilenga kuibua ukosefu wa usalama na vitisho vya usalama na wakati huo huo kuhalalisha siasa za chuki za Taliban dhidi ya maombolezo ya Muharram, siasa ambazo zimetekelezwa kupitia kukusanywa bendera na nembo za Muharram. Hii ni katika hali ambayo jamii ya Afghanistan inahitaji umoja wa kitaifa na kimadhehebu ili kuondokana na mzozo uliopo nchini humo. Hata hivyo, kadiri wakati unavyoendelea kupita ndivyo watu wa Afghanistan na jamii ya kimataifa inavyozidi kufahamu vizuri siasa na mipango halisi ya Taliban, jambo ambalo bila shaka katika kipindi cha muda mrefu halitakuwa na manufaa kwa kundi hilo.