Aug 06, 2022 10:48 UTC
  • China yamuwekea vikwazo Pelosi, yafuta baadhi ya ushirikiano na US

China imetangaza kuwa itasimamisha ushirikiano na Marekani katika mambo kadhaa hasasi, ukiwa ni muendelezo wa kujibu mapigo kwa ziara iliyofanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi katika kisiwa cha Taiwan hivi karibuni.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema, Beijing haitashirikiana tena na Marekani katika mambo kadhaa kama vile kupambana na jinai za mipakani, mabadiliko ya tabianchi, wahamiaji haramu na vita dhidi ya mihadarati miongoni mwa hatua nane ilizoziainisha.

Aidha China imetangaza kumuwekea vikwazo Spika wa Kongresi ya Marekani Nancy Pelosi na jamaa zake wa karibu, mbali na kusimamisha kwa muda mazungumzo baina ya Washington na Beijing katika masuala ya kijeshi.

Kadhalika Beijing imefuta mkutano wa pande mbili na Washington uliokuwa ufanyike karibuni hivi kujadili mikakati ya kuimarisha usalama wa vikosi vya majini vya Marekani na China.

Pelosi na maafisa wa serikali ya Taipei

Serikali ya Beijing imetangaza kuchukua hatua hizo wakati huu ambapo viokosi vyake vinaendelea kufanya mazoezi ya kijeshi katika maeneo sita yaliyo karibu na Taiwan, na ambayo yatamalizika kesho Jumapili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China inasisitiza kuwa, hatua ya Pelosi ya kuitembelea Taiwan ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya Jamhuri ya Watu wa China na vile vile ni ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Asia.

 

 

Tags