Aug 08, 2022 05:42 UTC
  • Ripoti ya Amnesty International kuhusu jinai za kivita za serikali ya Ukraine

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limetoa ripoti mpya na kuilaumu serikali ya Ukraine kwa jinai za kivita ilizofanya dhidi ya raia na watu wasio na hatia wa nchi hiyo.

Shirika hilo limesema kuwa, mbinu zinazotumiwa na jeshi la Ukraine ni uvunjaji wa sheria za kimataifa zinazowalinda raia. Miongoni mwa hila zinazotumiwa na jeshi la Ukraine kwa mujibu wa Amnesty International ni kuweka silaha katika kambi ambazo ziko katikati ya makazi ya watu na wakati kambi hizo zinaposhambuliwa, watu wa kawaida nao wanauawa na kujeruhiwa na makazi yao kuharibiwa.

Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty Internation amesema: Tuna ushahidi na vielelezo vya kutosha vinavyothibitisha kuwa wanajeshi wa Ukraine wanahatarisha maisha ya raia na wanavunja sheria za kimataifa katika vita wakati wa operesheni na mbinu zao za kivita. Kuwaweka wananchi wa Ukraine katika maeneo ya mapigano hatuwezi kamwe kusema ni kuwalinda wala hakuwezi kuwa ni kuheshimu sheria za kimataifa na haki za binadamu.

Vita nchini Ukraine

 

Hii ni mara ya kwanza kwa shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International kuishutumu rasmi serikali ya Ukraine kufanya jinai za kivita na kucheza na roho za raia na wananchi wa kawaida. Hadi hivi sasa nchi za Magharibi hususan Marekani zilikuwa zinafanya njama za kila namna za kuituhumu Russia kuwa ndiyo inayofanya jinai za kvita huko Ukraine na hasa baada ya kupatikana viwiliwili vya raia katika mji wa Bucha kwenye viunga vya Kyiv, mji mkuu wa Ukraine. Lakini viongozi wa ngazi za juu wa Russia pamoja na Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo wamekuwa wakikanusha mara kwa mara madai ya kuua raia huko Ukraine na wanasisitiza kuwa, jeshi la Ukraine na wanamgambo wenye fikra za Kinazi kama genge la Azov lenye misimamo mikali ndio wanaofanya jinai hizo na baadaye kuisingizia Russia. Moscow inasema, jeshi la Ukraine na magenge ya wanamgambo yenye fikra kali za Kinazi wanatanguliza mbele raia na kuwatumia wananchi wa kawaida kama ngao katika vita. Mara kwa mara Russia imekuwa ikisema pia kuwa, serikali ya Ukraine na wanamgambo wake wanaweka silaha katika maeneo ya raia ikiwemo mizinga na makombora ya ardhi kwa anga ili kutungua ndege za Russia na kila pale Moscow inapojibu mashambulizi kwa kupiga sehemu zilipo silaha hizo, Ukraine inalalamika kuwa Russia imeshambulia maeneo ya raia. 

Mikhail Mizintsev, Mkuu wa Kituo cha Ulinzi wa Taifa cha Russia anasema: Wanamgambo wa Ukraine wameweka kambi zao mashuleni na hata mahospitalini katika miji mbalimbali ya Ukraine

Vita vya Ukraine vimesababisha hasara kubwa

 

Si hayo tu, lakini pia wanamgambo wa genge la Kinazi na Kizayuni la Azov wana mchango mkubwa wa kuzuia wananchi wa Ukraine wasitoke kwenye miji yao wakiwemo wakazi wa mji wa Mariupol wakati ulipokuwa umezingirwa na wanajeshi wa Russia. Wanamgambo hao waliwatumia raia kama ngao yao vitani mbele ya mashambulio ya jeshi la Russia na kila mwananchi alipojaribu kutoroka, walikuwa wanawapiga risasi kwa madai ya kudumisha nidhamu.

Hivi sasa lakini Amnesty Internation imejitokeza hadharani na kuishutumu Ukraine kwa kutumia vibaya raia kwa kuwafanya ngao ya kivita. Ripoti ya shirika hilo imebainisha wazi kuwa, katika kipindi cha baina ya mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu wa 2022, wanajeshi wa Ukraine walitumia majengo ya makazi ya watu kama vituo vyao vya kijeshi vya kuwashambulia wanajeshi wa Russia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Amnesty Internation, miji na vijiji visivyopungua 19 vilishuhudia mbinu hizo za wanajeshi na wanamgambo wa serikali ya Ukraine za kutumia majengo ya makazi ya watu kama vituo vyao vya kijeshi. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Ukraine imeweka kwa uchache kambi tano za kijeshi katika mahospitali ya nchi hiyo kwenye kipindi cha baina ya mwezi Aprili na Juni mwaka huu. Cha kushangaza zaidi ni kuwa, ripoti ya wakaguzi na wataalamu wa Amnesty Internation inaonesha kwamba kati ya shule 29 zilizokaguliwa, 22 kati yake ziligeuzwa kambi za kijeshi na serikali ya Ukraine.

Serikali ya Ukraine inalaumiwa kwa kufanya raia ngao za kivita

 

Kama ilivyotarajiwa lakini, viongozi wa Ukraine wameilalamikia vikali ripoti hiyo akiwemo rais wa nchi hiyo, Volodymyr Zelenskyy na waziri wake wa mambo ya nje, Dmytro Kuleba. Swali la kujiuliza hapa ni kuwa, lau kama Amnesty Internation ingetoa ripoti kama hiyo dhidi ya Russia,  je, viongozi wa Ukraine wangelilituhumu shirika hilo kuwa halikufanya insafu?  

Tags