Aug 07, 2022 06:39 UTC
  • Russia: Tumeua makumi ya mamluki wa kigeni nchini Ukkraine

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limeua makumi ya mamluki wa kigeni katika shambulizi la anga dhidi ya kambi ya kijeshi ya kigeni nchini Ukraine.

Shirika la habari la TASS limemnuukuu Igor Konashenkov akisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, jeshi la Russia limeua zaidi ya mamluki 80 wa kigeni katika shamblio la anga dhidi ya kambi ya kijeshi ya kigeni kwenye mji wa Dnipro wa katikati ya Ukraine na kuangamiza silaha nyingi.

Tarehe 24 Februari mwaka huu wa 2022, Russia ilianzisha operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine kwa ombi la majimbo yaliyotangaza kujitenga na nchi hiyo, ya  Luhansk na Donetsk.

Igor Konashenkov

 

Tangu wakati huo, viongozi wa Russia wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa, kamwe hawashambulii miundombinu ya Ukraine, bali lengo lao ni kuipokonya silaha nchi hiyo, kupambana na magenge yenye misimamo mikali ya fikra za Kinazi na kuizuia Ukraine isiwe tishio kwa usalama wa Russia.

Pamoja na hayo nchi za Magharibi hususan Marekani zimeshadidisha vikwazo vyao vya kila namna dhidi ya Russia, zimepeleka silaha zao huko Ukraine kwa shabaha ya kuvifanya vita hivyo vichukue muda mrefu sana bila ya kujali maafa wanayopata wananchi wa Ukraine na zinazuia juhudi zote za kumaliza vita hivyo. 

Igor Konashenkov, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema, jeshi la anga la nchi hiyo limetungua pia ndege mbili za kivita za Ukraine aina ya Su-25 katika kipindi cha masaa 24.

Aidha amesema, jeshi la anga la nchi hiyo limetungua ndege 8 zisizo na rubani za Ukraine tangu Ijumaa ya wiki iliyopita hadi hivi sasa

Tags