Aug 08, 2022 06:37 UTC
  • Siku ya kukumbuka jinai za kivita za Marekani mjini Hiroshima na Nagasaki

Jumamosi, na ikiwa ni katika kukumbuka miaka 79 ya maafa ya atomiki ya Hiroshima, watu wa Japan waliwakumbuka maelfu ya wahanga wa shambulio hilo la atomiki la Marekani kwenye mji huo na mji mwingine wa Nagasaki.

Washiriki walikaa kimya saa 8:15 asubuhi, ikiwa ni muda ambao Marekani ilidondosha bomu la atomiki kwenye mji wa Hiroshima mnamo Agosti 6, 1945.

Mlipuko wa bomu la atomiki la Marekani huko Hiroshima na Nagasaki mnamo Agosti 6 na 9, 1945 uliua kinyama Wajapani 220,000.

Jinai hiyo ya Marekani inachukuliwa kuwa jinai kubwa zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya binadamu ambapo athari na matokeo yake yangali yanaendelea kuwasumbua watu wa Japan. Kila aina ya magonjwa ya ngozi, kupumua na ulemavu uliosababishwa na shambulio la atomiki la Marekani katika miji miwili hiyo ya Japan yalisababisha vizazi vilivyofuata vya watu wa Japan kuwa na ulemavu tofauti.

Japan ikiadhimisha kumbukumbu ya jinai ya Marekani huko Hiroshima na Nagasaki

Tadatoshi Ekiya, mtaalamu wa masuala ya kijamii nchini Japani, anasema: "Kuunda ulimwengu salama na wenye afya kunahitaji kutokomezwa silaha za nyuklia, na serikali ya Japan lazima pia ikomeshe makubaliano ya mwavuli wa nyuklia wa Amerika ili kuhakikisha usalama wa watu wa Japan."

Wakati Marekani inazituhumu nchi nyingine kuwa zinahatarisha usalama wa dunia kutokana na mipango yao ya nyuklia, yenyewe ni nchi ya kwanza kuwahi kutumia bomu la atomiki dhidi ya watu wasio na hatia. Kinachowakasirisha zaidi watu wa Japan ni kwamba wahusika wa jinai hiyo ya kutisha hawakuchukuliwa hatua katika mahakama yoyote ya sheria na serikali ya Marekani ingali inaendelea kutetea jinai hiyo kwa visingizio mbalimbali.

Serikali ya Japan inaendelea kuunga mkono waziwazi ulimwengu usio na silaha za nyuklia, na maonyesho ya athari za mashambulizi ya nyuklia ya Marekani huko Hiroshima na Nagazaki ni uthibitisho wa wazi na hai kuhusu jinai zilizofanywa na nchi hiyo ya Magharibi dhidi ya binadamu, jinai ambazo zinapasa kuifanya iaibike mbele ya macho ya walimwengu.

John Hersey, mtaalamu na mwandishi wa habari wa Marekani, alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kufika katika eneo la tukio baada ya shambulio la nyuklia la Marekani, na picha alizopiga zimerekodi na kuanika wazi kina cha maafa ya binadamu na jinai zilizotekelezwa na serikali na jeshi la Marekani katika uwanja huo.

Ushahidi wake kuhusu jinai hiyo ambayo iliakisiwa pakubwa katika vyombo vya habari vya dunia, uliufahamisha ulimwengu kuhusu kina cha jinai zinazofanywa na Marekani katika pembe tofauti za dunia.

Mhanga wa bomu la nyuklia la Marekani mjini Hiroshima

Kwa vyovyote vile, kukumbukwa jinai iliyofanywa na Marekani huko Hiroshima na Nagasaki ni mapitio ya jinai iliyotekelezwa na nchi hiyo nchini Japan, jinai ambayo inaweza kutokea tena katika nchi nyingine yoyote duniani. Kwa sababu hiyo, ulimwengu ukiwa unafungamana na watu wa Japan katika kukumbuka siku hiyo ya huzuni na majonzi, unataka kuwepo dunia isiyo na silaha za nyuklia. Historia inaonyesha kuwa kujirundikia silaha za nyuklia sio tu hakuleti usalama, bali pia huzidisha wasiwasi wa kimataifa kuhusu kujirudia matukio na jinai kama ile ya shambulio la bomu la nyuklia la Marekani huko Hiroshima na Nagasaki. Pamoja na hayo lakini Marekani kutokana na kiburi na bila kujali lolote, inaendelea kuongeza maghala yake ya silaha za nyuklia, na suala hilo bila shaka linahatarisha zaidi usalama wa jamii ya kimataifa.