Aug 09, 2022 02:54 UTC
  • Russia: Tutafanya suluhu na Ukraine kwa masharti yetu, si kwa masharti ya Magharibi

Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesisitiza kuwa uamuzi wa kuliunganisha eneo la Crimea na Russia ilikuwa hatua sahihi kabisa kwa sababu uliifanya Russia iwe imara zaidi na vilevile uliwasaidia watu wa Crimea.

Dmitry Medvedev amesema: "Rais Vladimir Putin wa Russia alichukua uamuzi pekee ambao iliwezekana kuuchukua kuwasaidia watu wa Crimea, kwa kuliunganisha eneo hilo na Russia. Inapasa nikumbushe pia kuwa, hatua hiyo ambayo iliungwa mkono pia na akthari mutlaki ya wakazi wa Crimea ilichukuliwa kulingana na sheria za kimataifa. Tulichukua hatua sahihi. Tuliwasaidia watu wa Crimea na wakati huohuo tuliimarisha zaidi nchi yetu."

Medvedev amesisitiza pia kuwa, Russia haitafanya suluhu na Ukraine isipokuwa kwa masharti ambayo yatatolewa na Moscow yenyewe.

Akifafanua zaidi, Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema: "Russia inaendelea na operesheni maalumu ya kijeshi ndani ya Ukraine na inataka kufikia suluhu itakayoendana na masharti yake, si masharti wanayotaka washirika wetu wa zamani wa kimataifa. Wao wanataka jeshi la Russia lishindwe ili waweze kutubebesha masharti yao."

 

Tarehe 24 Februari mwaka huu, jeshi la Russia liliishambulia kijeshi Ukraine kuitikia ombi la viongozi wa maeneo ya Luhansk na Donetsk la kupatiwa msaada wa kukabiliana na mashambulio ya Kyiv.

Tangu wakati huo, viongozi wa Moscow wameeleza mara kadhaa kwamba jeshi la nchi hiyo halitailenga kwa namna yoyote ile miundomsingi ya kiraia nchini Ukraine na wala halitaikalia kijeshi nchi hiyo na kwamba linachofuatilia ni kutokomeza Unazi na kuipokonya Ukraine silaha.

Kwa upande wao, nchi za Ulaya na Magharibi na hasa Marekani zimekuwa zikishadidisha mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Russia kwa kupeleka Ukraine aina mbalimbali ya silaha nyepesi na nzito.

Hatua hiyo si tu haijasaidia kuhitimisha vita vya Ukraine bali imechochea na kukoleza zaidi moto wa vita na mapigano nchini humo.../