Aug 10, 2022 01:21 UTC
  • Taiwan yadai kuwa China inataka kuivamia kijeshi

Taipei imedai kuwa China inapanga njama ya kukivamia kisiwa cha Taiwan, baada ya Beijing kutangaza duru mpya ya mazoezi ya kijeshi katika maji ya kisiwa hicho, ukiwa ni muendelezo wa kujibu mapigo kwa ziara iliyofanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi katika kisiwa hicho hivi karibuni.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Taiwan, Joseph Wu amesema, China inatumia luteka hizo za kijeshi kando kando ya Taiwan kwa ajili ya kujiandaa kukivamia kijeshi kisiwa hicho.

Wu amedai kuwa, "China inafanya mazoezi makubwa ya kijeshi, inavurumisha makombora, inafanya mashambulio ya kimtandao, inapotosha taarifa, na kutumia mashinikizo ya kiuchumi ili kudhoofisha ari ya umma Taiwan."

Haya yanajiri siku chache baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China kusema, Beijing haitashirikiana tena na Marekani katika mambo kadhaa kama vile kupambana na jinai za mipakani, mabadiliko ya tabianchi, wahamiaji haramu na vita dhidi ya mihadarati miongoni mwa hatua nane ilizoziainisha.

Spika Pelosi akiwa Taiwan

Aidha China imetangaza kumuwekea vikwazo Spika wa Kongresi ya Marekani Nancy Pelosi na jamaa zake wa karibu, mbali na kusimamisha kwa muda mazungumzo baina ya Washington na Beijing katika masuala ya kijeshi.

China inasisitiza kuwa, hatua ilizochukua ni jibu kwa kitendo cha Pelosi cha kuitembelea Taiwan mapema mwezi huu, na kwamba ziara hiyo ilikuwa uingiliaji wa masuala ya ndani ya Jamhuri ya Watu wa China mbali na kukiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Asia.

Tags