Aug 10, 2022 05:28 UTC
  • Mwaka mmoja wa utawala wa Taliban nchini Afghanistan

Mwaka mmoja umepita tangu kundi la Taliban lilipoingia tena madarakani nchini Afghanistan lakini inaonekana kuwa mateso na matatizo ya wananchi yameongezeka kuliko hata wakati nchi hiyo ilipokuwa inakaliwa kwa mabavu na Marekani na NATO katika miaka ya 2001 hadi 2021.

Mwezi Agosti 2021, kundi la Taliban lilichukua tena madaraka ya Afghanistan na kuahidi kuwa litawapunguzia wananchi wa nchi hiyo mateso na matatizo. Waliahidi kuwa utawala wao utahakikisha kwamba roho na mali za wananchi wa Afghanistan zinalindwa na watatambua rasmi uhuru wao.

Unapoyaangalia matamshi ya msemaji wa kundi la Taliban, Zabiullah Mujahid, katika mazungumzo yake ya kwanza kabisa na waandishi wa habari baada ya kupinduliwa serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani na kuingia tena madarakani kundi hilo huko Afghanistan utaona kuwa, Taliban hawajatekeleza ahadi zao hata moja zilizotangazwa na Mujahid wakati huo, bali baadhi ya wakati kundi hilo hata linakwenda kinyume na ahadi zake.

Kundi la Taliban liliwaahidi wananchi wa Afghanistan kuwa litawaletea maisha mazuri, lakini mwaka mzima umepita na ndio kwanza maisha ya wananchi wa Afghanistan yanazidi kuwa magumu siku baada ya siku.

Zabiullah Mujahid

 

Mfumuko wa bei umepanda vibaya nchini Afghanistan. Ughali wa maisha ni mkubwa kiasi kwamba mashirika ya misaada ya kibinadamu yametabiri kutokea mgogoro mkubwa wa kibinadamu kutokana na ukame pamoja na njaa kwa mamilioni ya Waafghani.

Kundi la Taliban liliwaahidi wananchi wa Afghanistan kuwaimarishia usalama wao jambo ambalo ni la kimsingi kabisa kwa kila jamii, hususan jamii za wachache. Lakini mwaka mzima umepita na si tu usalama ni mdogo bali wigo wa vitisho vya kiusalama nao umezidi kuwa mpana hususan dhidi ya watu wa dini na kaumu za watu wachache.

Kwa upande wa jamii za wanawake pia, kundi la Taliban liliahidi kwamba litaheshimu haki zao kwa uchache katika msingi wa sheria za Kiislamu. Lakini katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Taliban, wanawake wa Afghanistan si tu hawajapata haki zao kama unavyosema Uislamu lakini pia serikali ya Taliban inawanyima hata haki yao ya kupata elimu.

Licha ya dini tukufu ya Kiislamu kutilia mkazo mno wajibu wa kutafuta elimu tena bila ya kubagua baina ya mwanamme na mwanamke, lakini katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake, kundi la Taliban limewanyima haki zao za elimu wanawake wa nchi hiyo kwa madai yasiyo na msingi na pia limewapiga marufuku kushiriki katika harakati za kijamii ambazo hata Uislamu hauzipingi.

Hali ya kimaisha ni nzito na ngumu sana Afghanistan

 

Mwaka mmoja nyuma, msemaji wa kundi la Taliban aliahidi kwamba kundi hilo litaruhusu vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru. Lakini miezi 12 imepita ya utawala wa Taliban na vyombo vya habari vimezidi kubanwa kwa sheria kali kiasi kwamba tasnia ya uandishi wa habari nchini Afghanistan imo hatarini hivi sasa.

Aidha kutokana na mashinikizo ya jamii ya kimataifa, serikali ya Taliban iliahidi kuunda serikali itakayowakilisha watu wote nchini Afghanistan. Lakini katika kipindi chote hiki cha mwaka mmoja, kundi hilo halijachukua hatua zozote za kutekeleza kivitendo ahadi yake hiyo bali hata inashikilia nchi hiyo kutawaliwa na watu wa kundi na kaumu moja tu. Hali hiyo imepelekea dunia nzima iwe na msimamo mmoja kuhusu serikali hiyo ya Taliban. 

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Afghanistan, Andreas von Brandt  amesema kuwa, hivi sasa, jamii ya kimataifa inaafikiana katika suala la kutoitambua rasmi serikali ya Taliban. Amesisitiza pia kwa kusema: Serikali jumuishi na demokrasia nchini Afghanistan ndivyo vinavyohitajika kwa ajili ya kutambuliwa rasmi kundi hilo kama serikali.

Kiujumla ni kwamba hakuna ishara zozote za kupungua masaibu na mateso ya wananchi wa Afghanistan maadamu kundi la Taliban linaendelea kukataa kutekeleza ahadi zake na halitaki kuunda serikali inayowakilishwa na watu wote nchini humo.

Tags