Aug 10, 2022 07:46 UTC
  • China: Lengo la luteka ni kutoa onyo kwa Marekani na somo kwa wanaotaka kujitenga

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amesema, lengo la Beijing kufanya mazoezi ya kijeshi kandokando ya Taiwan ni kutoa onyo kwa Marekani na somo kwa wale wanaotaka kisiwa hicho kijitenge na China.

Wang Wenbin amebainisha kuwa, Beijing inaendelea na mazoezi ya kijeshi kandokando ya Taiwan ili kuipa onyo na indhari Marekani na kutoa funzo na somo kwa wanaotaka kisiwa cha Taiwan kijitenge na China.

Wenbin ameongezea kwa kusema: hatua tulizochukua kujibu safari ya pupa aliyofanya Nancy Pelosi, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Taiwan ni halali kisheria na zinakubalika kikamilifu. Hili ni onyo kwa wanaofanya chokochoko na somo kwa wanaotaka kujitenga.

Wang Wenbin

 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amesisitiza pia kuwa, kuna China moja tu, na Taiwan ni sehemu yake isiyoweza kutenganika nayo.

Siku moja mara baada ya safari ya Pelosi mjini Taipei, vikosi vya ulinzi vya China vilianza kufanya mazoezi ya kijeshi kwa kutumia zana halisi za kivita katika maeneo sita yanayozunguka kisiwa cha Taiwan.

Katika luteka hiyo, vikosi vya makombora vya jeshi vilifyatua makombora kadhaa yaliyolenga eneo la mashariki ya pwani ya Taiwan.

Beijing, ambayo ilikuwa imetishia kwamba safari ya Pelosi Taiwan itakuwa na matokeo mabaya, inasisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China na haijafuta uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi ili kushika hatamu za udhibiti wa kisiwa hicho.../