Aug 11, 2022 11:01 UTC
  • Korea Kaskazini yadai Korea Kusini imeienezea COVID

Mvutano umezuka kati ya Korea mbili kuhusu chanzo cha maambukizi ya COVID-19 Kaskazini, huku dada mwenye ushawishi wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un akiishutumu Kusini kwa kusababisha mlipuko huo nchini mwake na kuonya "kulipiza kisasi chenye kusababisha mauti. "

Katika hotuba yake, Kim Yo-jong aliilaumu Korea Kusini kwa kueneza COVID-19 Kaskazini kwa kutuma vipeperushi dhidi ya Pyongyang katika mpaka wa nchi mbili, na kutaja kitendo hicho kuwa ni "uhalifu dhidi ya ubinadamu."

Shirika la Habari la Korea (KCNA) liliripoti Alhamisi habari hiyo na kuongeza kuwa, alitaja "hatari ya kueneza ugonjwa wa kuambukiza kupitia vitu vilivyoambukizwa," akionya kwamba Pyongyang ilikuwa inazingatia "jibu kali la kulipiza kisasi."

"Hatuwezi tena kupuuza kuingia kwa taka bila kukatizwa kutoka Korea Kusini," alisema, na kutishia "kuwafuta" wakuu wa Seoul ikiwa shughuli hizo zitaendelea.

Korea Kusini imebainisha masikitiko yake juu ya matamshi ya Kim Yo-jong, na kuyataja kama "yasiyo na msingi."

"Tunaelezea masikitiko makubwa juu ya Korea Kaskazini mara kwa mara kutoa madai yasiyo na msingi kuhusu namna COVID ilivyoenea na kutoa matamshi ya dharau na ya kutisha," Wizara ya Muungano ya Korea Kusini imesema katika taarifa.

Kiongozi wa Korea Kaskazini  Kim Jong-un

Maoni ya Kim Yo-jong yamekuja wakati kaka yake akitangaza ushindi katika vita dhidi ya ugonjwa "mbaya" wa virusi vya COVID, na kuamuru vizuizi vya janga hilo, vilivyowekwa mnamo Mei, viondolewe. Kim Jong-un ametoa tangazo hilo katika mkutano na wafanyikazi wa afya na wanasayansi. Mkutano huo ulikuwa umeitishwa Jumatano kutathimini  namna nchi hiyo ilivyokabiliana na janga, akisisitiza kwamba Korea Kaskazini lazima idumishe "kizuizi chenye nguvu cha chuma cha kupambana na janga na kuzidisha kasi ya kupambana na janga hadi mwisho wa mgogoro wa afya duniani."

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amezidi kupongeza mafanikio ya nchi hiyo katika kukabiliana na kuenea ugonjwa huo kwa muda mfupi, na kuutaja kuwa ni "muujiza wa ajabu" ambao ungerekodiwa katika historia ya afya ya umma duniani.

Korea Kaskazini ilitangaza mlipuko wake wa kwanza wa COVID mnamo Mei na imeripoti maambukizo ya homa na vifo tangu wakati huo.