Aug 12, 2022 06:36 UTC
  • Onyo la jeshi la China kwa chokochoko za Taiwan

Jeshi la China limekionya kisiwa cha Taiwan dhidi ya kuendeleza chokochoko katika eneo hilo la kistratijia.

Katika taarifa, Kamandi ya Mashariki ya Jeshi la China imeonya kwamba vikosi vya nchi hiyo vitaendelea kuwa tayari kwa ajili ya vita huku vikiendelea kufanya mazoezi karibu na kisiwa cha Taiwan.

Kamandi ya Mashariki ya Jeshi la China imesema kwamba vikosi vya nchi hiyo vinafuatilia kwa karibu matukio katika Lango-Bahari la Taiwan, kufanya doria za mara kwa mara, na kuendelea na mafunzo ya kijeshi ili kuwa tayari kwa ajili ya vita.

China inasema madhumuni ya mazoezi yake ya kijeshi kukizunguka kisiwa cha Taiwan ni kuionya Marekani na kutoa somo kwa watu wanaotaka kukitenga kisiwa cha Taiwan na ardhi-mama ya China.

Safari ya karibuni ya Nancy Pelosi huko Taiwan iliyoibua mvutano kati ya kisiwa hicho na China

Wakati huohuo, manowari kadhaa za wanamaji wa China zimeendelea kushiriki katika luteka kwenye pwani ya mashariki ya Taiwan, jambo ambalo limezipelekea meli za kivita za Taiwan nazo zijiandae kwa ajili ya vita.

Mpango wa jeshi la China wa kuwabakisha askari wake wanaoshiriki katika mazoezi ya hivi sasa katika Lango-Bahari la Taiwan, hata baada ya kumalizika mazoezi hayo ya kijeshi kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa awali, unaonyesha kuwa mvutano kati ya Beijing na Taipei utaendelea kwa miezi michache ijayo.

Mvutano kati ya China na Taiwan ulifikia kilele siku chache zilizopita baada ya Nancy Pelosi, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kuchukua uamuzi wa kusafiri Taipei na kuzungumza na baadhi ya viongozi wa kisiwa cha Taiwan, katika hatua ya kutatanisha iliyokwenda kinyume na kanuni ya China Moja.

Jeshi la China lilianza kufanya mazoezi katika Lango Bahari la Taiwan wakati huo huo wa kufanyika safari ya Pelosi huko Taiwan, ambapo viongozi wa Beijing walisema ni onyo na somo kwa wale wanaotaka kukitenga kisiwa hicho na vile vile kwa viongozi wa Ikulu ya White House.

Kwa kuzingatia kwamba mzozo kati ya China na Taiwan ungali unaendelea, kuna swali kuwa je, mvutano huo ambao unaweza kugeuza mwelekeo wa uchumi wa China, utaendelea hadi lini na marekebisho ya uhusiano wao yatafanyika kwa msingi gani?

Harris Templeman, mtaalamu wa masuala ya siasa katika chuo kikuu cha Stanford anasema kurejesha uwiano kati ya China na Taiwan kunahitaji diplomasia ngumu. Sijui mvutano huo utaishia wapi, lakini kwa maoni yangu tungali tuna wiki chache ngumu mbele yetu.

Kuna fikra hii kwamba sera ya China ya kukabiliana vilivyo na wale wanaotaka kujitenga kisiwani Taiwan na wanaokiuka msingi wa China Moja kikanda na kimataifa ni mkakati ambao viongozi wakuu wa Beijing wameuweka kwenye ajenda ya kulinda mamlaka yao ya kitaifa, ambapo sehemu kubwa ya mkakati huo ni kuifikishia Marekani ujumbe madhubuti, nchi ambayo daima inafanya juhudi za kuvuka mistari myekundu ya Beijing.

Luteka ya China karibu na kisiwa cha Taiwan

Harsh V Pant, mchambuzi wa sera za kigeni wa Taasisi ya Utafiti ya Observer, anasema: Xi Jinping hataki kuonekana kuwa kiongozi anayeonyesha dalili za udhaifu anapoingia katika muhula wake wa tatu ambao haujawahi kushuhudiwa tena nchini China, na anataka kuingia katika historia ya kuwa kiongozi aliyeiunganisha Taiwan na China. Bila shaka jambo hilo litaigharimu zaidi Taiwani.

Inaonekana mvutano kati ya China na Taiwan hautavuka kiwango cha sasa, kwa sababu kuendelea kwake kunaweza pia kuisababishia Beijing matatizo makubwa, kwa kutilia maanani kuwa ina ushindani mkubwa wa kiuchumi na Washington, na Taiwan nayo haiko tayari kukabiliana na matokeo yasiyotabirika ya jaribio lolote la kuongezeka hasira ya Beijing katika uwanja huo.

Tags