Aug 12, 2022 12:11 UTC
  • Russia: Hatima ya Zelensky ni kupandishwa kizimbani au kurudi kwenye uchekeshaji

Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ametabiri kuwa mustakabali na hatima ya rais Vlodomyr Zelensky wa Ukraine itakuwa ni kupandishwa kizimbani au kurejea kwenye tasnia ya uchekeshaji wa usanii wa Kimagharibi.

Dmitry Medvedev, ambaye amelitembelea eneo la Luhansk, mashariki ya Ukraine, mbali na kueleza utabiri huo kuhusu hatima ya rais wa Ukraine amefanya mkutano pia na viongozi wa eneo hilo na jengine la Donetsk lililoko mashariki ya nchi hiyo na kuzungumzia hatua za vipaumbele vya kiusalama zinazopasa kuchukuliwa katika maeneo hayo.

Rais huyo wa zamani wa Russia amesema, sababu ya kufanya ziara katika eneo la Luhansk ni “kutoa ulinzi bora kwa wakazi wa Donbass na maeneo mengine yaliyokombolewa”.

Dmitry Medvedev

 

Aidha, mapema kabla ya hapo, Medvedev alitoa jibu pia kwa kauli ya rais Vlodomyr Zelensky wa Ukraine aliyekuwa amezitolea mwito nchi zote za Magharibi ziwapige marufuku raia wote wa Russia kwa kusema, fikra, mienendo na misimamo ya kiongozi huyo inafanana na ya mtawala wa zamani wa Ujerumani ya Manazi, Adolf Hitler.

Medvedev alieleza bayana kuwa, Zelensky anatekeleza siasa zile zile za Adolf Hitler, kiongozi wa zamani wa Kinazi nchini Ujerumani, kwa kutaka kuadhibiwa wananchi wote wa Russia.

Katika kauli yake Zelensky alisema, Warusi wote bila kujali misimamo na itikadi zao za kisiasa wanapaswa kufukuzwa katika nchi za Magharibi haraka iwezekanavyo, na nchi hizo pia zisiwapokee raia wengine kutoka Russia…/