Aug 13, 2022 01:30 UTC
  • China: Vikwazo vya US vimeisababishia Iran hasara ya dola bilioni 200

China imesema vikwazo haramu na vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran vimelisababishia taifa hili la Kiislamu hasara ya mabilioni ya dola.

Lijian Zhao, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameashiria ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani katika nchi za eneo la Asia Magharibi na kwengineko na kueleza kuwa, vikwazo vilivyowekwa na utawala wa Donald Trump, aliyekuwa rais wa Marekani dhidi ya Iran vimeusababishia uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu hasara ya dola bilioni 200.

Ikumbukwe kuwa, serikali ya Trump mwaka 2018 ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyopasishwa mwaka 2015, na kisha kutangaza vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Tehran.

Mapema mwezi huu pia, Fu Cong, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Silaha katika Wizara ya Mambo ya China aliitaka Marekani iiondolee Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo haramu.

Alisisitiza kuwa, pande zote za makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zinapaswa kujitolea kwa dhati kuhakikisha kuwa mapatano hayo ya kimataifa yanarejea katika mkondo kupitia mazungumzo ya kidiplomasia, na kujiepusha na tabia ya kushinikiza kupitia vikwazo na vitisho vya kutumia nguvu.

 

 

Tags