Aug 13, 2022 07:58 UTC
  • Nyaraka 11 zikiwemo za

Wakati aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump anakanusha kuweka nyumbani kwake nyaraka zozote zinazohusu masuala ya nyuklia, polisi ya upelelezi ya nchi hiyo FBI imetangaza kuwa imekuta na kukamata jumla ya nyaraka 11 za siri nyumbani kwa kiongozi huyo mjini Mar-a-Lago, Florida.

Siku ya Jumanne iliyopita, Trump alitangaza kuwa kasri lake la Florida limezingirwa, kuvamiwa na kudhibitiwa na kundi kubwa la maafisa wa FBI, ambao wamepekua hata sanduku lake la kuhifadhia vitu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, gazeti la Wall Street limeripoti kuwa, katika uvamizi iliofanya siku ya Jumatatu katika makazi ya Mar-a-Lago jimboni Florida, FBI ilikuta na kunasa maboksi yapatayo 20 ya nyaraka zikiwemo nyaraka 11 za siri.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo, Polisi ya Upelelezi ya Marekani iligundua na kukamata karibu maboksi 20 ya nyaraka zikiwemo za picha, waraka wa maandishi ya mkono ambao haujulikani unahusu kitu gani, dikrii au amri ya utekelezaji ya Trump ya kutoa msamaha kwa Roger Stone na taarifa kuhusu rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Gazeti la Wall Street limebainisha kuwa FBI imekamata pia maboksi matatu ya nyaraka za siri zikiwemo ndani yake nyaraka za siri kubwa.

Wakati huohuo tovuti ya habari ya Politico imeripoti kuwa Polisi ya Upelelezi ya Marekani inafanya uchunguzi dhidi ya Trump kwa sababu ya kuteketeza nyaraka, kuweka vizuizi vya kukwamisha uchunguzi na kukiuka sheria ya ujasusi ya nchi hiyo.../