Aug 13, 2022 08:06 UTC
  • Waturuki watabiri mwisho wa enzi za kisiasa za Erdogan

Viongozi wa aghalabu ya vyama vya siasa nchini Uturuki wametabiri kuwa mgogoro wa hali mbaya ya uchumi sambamba na sera mbovu za Rais Recep Tayyip Erdoğan za kujichukulia maamuzi kivyake pamoja na kuingilia kila jambo vitahitimisha enzi za kisiasa za kiongozi huyo.

Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa, chunguzi nyingi za maoni zilizofanywa ndani ya Uturuki zinaonyesha kwamba, chama tawala cha Uadilifu na Ustawi, ambacho huko nyuma kilikuwa kikijizolea zaidi ya asilimia 50 ya kura za wananchi, hivi sasa kinapoteza umaarufu wake kwa kufikia kiwango cha chini ya asilimia 30.

Na ni kwa sababu hiyo, viongozi wa aghalabu ya vyama vya siasa nchini Uturuki wametabiri kuwa mgogoro wa hali mbaya ya uchumi sambamba na sera mbovu za Rais Recep Tayyip Erdoğan za kujichukulia maamuzi kivyake pamoja na kuingilia kila jambo vitahitimisha maisha ya kisiasa ya kiongozi huyo.

Erdogan

 

Kiongozi wa chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Saadat Temel Karamollaoğlu yeye anaamini kwa dhati kuwa Erdogan na chama chake wanadhoofika na kuporomoka kisiasa.

Karamollaoğlu amesema, Erdoğan ambaye tangu alipotwaa madaraka hadi sasa amekuwa katika ulingo wa siasa kwa muda wa miaka 30, kuanzia wakati aliposhika wadhifa wa kiongozi wa tawi la vijana la chama cha Kiislamu cha Refah cha hayati Erbakan, na umeya wa jiji la Istanbul, hivi sasa ameshafika ukingoni kiasi kwamba hataweza kuendelea na siasa hata kwa sura ya kuwa kiongozi wa upinzani.

Mehmet Tezkan, mchambuzi na mwandishi wa habari ametabiri kuhusu uchaguzi mkuu wa Uturuki utakaofanyika mwakani akisema, "ikiwa uchaguzi huo utafanyika Erdogan atapaswa kufunga virago na kuhama Ikulu ya Beştepe. Erdogan anaendelea kuporomoka. Haya si maneno na uchambuzi wangu mimi, ni ukweli unaoonyeshwa na chunguzi za maoni".../

 

Tags