Aug 13, 2022 08:13 UTC
  • Russia yaonya juu ya uwezekano wa kuvunja uhusiano na Marekani

Afisa mmoja katika wizara ya mambo ya nje ya Russia ameonya kuwa uhusiano wa nchi hiyo na Marekani unaweza ukafika kwenye "nukta isiyoweza kurudishika nyuma" na mbaya zaidi kuliko ya hivi sasa.

Alexander Darchiev, mkuu wa idara ya Amerika Kaskazini katika wizara ya mambo ya nje ya Russia amesema, ikiwa Seneti ya Marekai itapitisha mipango inayolenga kuitambulisha Russia kuwa ni nchi inayofadhili ugaidi, hatua hiyo itamaanisha kuwa Washington imeshavuka nukta isiyoweza kurudishika nyuma.

Darchiev ameendelea kueleza kwamba, hatua hiyo "itasababisha madhara makubwa zaidi kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili, na kufikia hatua ya kupunguzwa au hata kuvunjwa kikamilifu".

Kabla ya hapo balozi wa Russia mjini Washington alitangaza kuwa, Marekani haijaonyesha utayarifu wake wa kuanzisha tena mazungumzo ya uthabiti wa kistratejia, lakini Moscow iko tayari kusubiri hadi upande wa Marekani utapofikia kwenye ukomavu wa kufanya hivyo.

 

Siku ya Jumatano iliyopita, Seneti ya Marekani ilipitisha kwa kauli moja azimio linalomtaka waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Antony Blinken aitangaze Russia kuwa ni nchi inayofadhili ugaidi kwa sababu ya hatua inazochukua Chechnya, Georgia, Syria na Ukraine.

Hata hivyo hadi sasa Blinken hajaonyesha nia yoyote ya kufuatilia suala hilo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, siku ya Alkhamisi, bunge la Lithuania lilitoa taarifa kupitia tovuti yake rasmi ambayo imeitambua Russia kuwa ni nchi inayofadhili na kuunga mkono ugaidi.../ 

Tags