Aug 13, 2022 11:21 UTC
  • Marekani imeanzisha vita 400, robo barani Afrika na Asia Magharibi

Utafiti mpya umefichua kuwa, zaidi ya robo ya vita vilivyoanzishwa na Washington katika historia ya Marekani vimefanyika katika nchi za Afrika na eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Utafiti huo uliopewa anuani isemayo: Mradi wa Uingiliaji wa Kijeshi, Data Mpya za Uingiliaji wa Kijeshi wa Marekani, umeonesha kuwa, Marekani imeanzisha vita mara 400 baina ya mwaka 1776 na 2019, huku asilimia 25 ya vita hivyo vikifanyika baada ya kipindi cha Vita Baridi.

Utafiti huo umebainisha kuwa, Marekani ilishadidisha uingiliaji wake wa kijeshi katika nchi za Afrika na eneo la kistratajia la Asia Magharibi, baada ya mashambulizi ya Septemba 11.

Sidita Kushi, Profesa Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Bridgewater huko Massachusetts nchini Marekani, ambaye ni mmoja wa waandishi wa utafiti huo amesema, hawakutarajia uingiliaji wa kijeshi wa Marekani katika nchi mbalimbali duniani uwe wa kiasi kikubwa kama ilivyobainishwa na data walizokusanya.

Ripoti ya utafiti huo imeeleza kuwa, baada ya kuanguka kwa Umoja wa Sovieti mwaka 1991 na Marekani kuwa nguvu kubwa ya kijeshi duniani, lakini hilo halikupunguza uchu wa Washington wa kuendelea na uingiliaji wake wa kijeshi katika kona mbaimbali za dunia.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), Marekani hutenga dola bilioni 800 kila mwaka kwa ajili ya masuala ya kijeshi, hiyo ikiwa ni asilimia 40 ya bajeti za majeshi yote kote duniani kwa mwaka.

Tags