Aug 14, 2022 02:27 UTC
  • Nyayo za mafia Waisraeli katika madai  ya Wizara ya Sheria ya Marekani dhidi ya IRGC

Wizara ya Sheria ya Marekani imechapisha taarifa inayodai kuwa mtu mmoja kwa jina Shahram Poursafi, ambaye wizara hiyo ilimtaja kuwa mwanachama wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), alipanga kumtumia Mmarekani mmoja kumuua John Bolton na afisa mwingine wa utawala wa Donald Trump.

Madhumuni ya njama hiyo imetajwa kuwa ni kulipiza kisasi mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Luteni Jenerali Hajj Qassem Soleimani, ambayo yalitekelezwa kwa amri ya moja kwa moja ya Trump.  Lakini ukweli ni kwamba katika siku chache za kwanza za kuuawa shahidi kamanada huyo, kutokana na hisia za mamilioni ya Wairani waliokasirishwa na kitendo hicho na waliotaka kulipizwe kisasi, Iran ilichukua hatua ya kulilipiza kisasi kwa kuvurimisha makombora yaliyolenga makao makuu ya jeshi la Marekani katika kambi ya Ain al-Assad nchini Iraq, ambayo ni mahali ambapo ndege isiyo na rubani ya  Marekani ilitokea na kumuua shahidi Soleimani. Hadi sasa wanajeshi wa Marekani wangali wanasakamwa na jinamizi la kutisha la oparesheni hiyo ya ulipizaji kisasi.

Kwa kuzingatia hilo, swali linalopaswa kuulizwa ni hili kuwa, je, ni malengo gani yanafuatiliwa na Wizara ya Sheria ya Marekani katika kutoa madai hayo yasiyo na msingi? Na je, Wizara ya Sheria ya Marekani kimsingi ni mhusika huru katika kesi hiyo, au imetoa madai hayo chini ya mashinikizo ya baadhi ya taasisi za usalama na kijasusi au makundi mengine ya mashinikizo?

Kwa upande wa maudhui, kabla ya kufanana na maandishi ya mahakama adilifu, madai ya Wizara ya Sheria ya Marekani yanaonekana kuwa sawa na mpango ulioratibiwa na shirika la kijasusi la Marekani la CIA miaka michache iliyopita kuhusu njama za kutaka kuuawa Adel Jubeir, balozi wa wakati huo wa Saudi Arabia huko Washington, au madai ya miezi michache iliyopita ya shirika la kijasusi la Israel, Mossad ambalo liishutumu IRGC kuwa ilipanga kuwaua raia watatu wa Marekani, Ufaransa na Uturuki kwa wakati mmoja lakini baadaye ikabainika kuwa mtu ambaye alidaiwa kuwa alipanga kutekeleza njama hiyo alikuwa ametekwa nyara na Mossad na kulazimishwa kukiri kuhusu suala hilo.

Uchapishaji wa madai hayo wakati huu unaonekana kuhusiana na angalau masuala mawili ambayo vyombo vya habari vya Magharibi vimekataa kuyataja. La kwanza ni mazungumzo ya hivi karibuni kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ambayo yalianza tena kwa kuzingatia pendekezo la Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya. Upande wa Iran ulikuwa bado unasubiri kurejea mazungumzo baada ya Ashura ili kufikia mapatano ya mwisho. Sasa pande ambazo zimekuwa zikishinikiza nchi za Magharibi ziachane na mazungumzo hayo kuhusu kuhuishwa JCPOA zinaonekana kushirikiana na Wizara ya Sheria ya Marekani katika kuwasilisha madai mapya ili kuvuruga mazungumzo hayo ya Vienna. Hakuna shaka kuwa njama hizi zinatekelezwa na mamafia Waisraeli na Kizayuni ambao kwa mara nyingine wamechukua hatua hiyo nchini Marekani kutokana na uchaguzi wa katikati ya muhula wa Congress.

Pili ni kuingia kwa uchumi wa Marekani katika kipindi cha mdororo, jambo ambalo limeifanya serikali ya chama cha Democratic cha Biden kugeukia masuala ya usalama ili kupotosha fikra za umma kuhusu maswala ya kiuchumi ya ndani. Hii ni mbinu ambayo pia hutumiwa na chama cha Republican. Ikiwa ni katika kufanikisha sera hizo za kupotosha fikra za umma serikali ya Biden imetangaza kumuua Ayman al-Zawahiri ili kuwavuatia Wakristo wenye misimamo mikali kama vile Bolton na waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Trump Mike Pompeo. Hatua hizo zimechukuliwa ili pengine kupunguza mashinikizo dhidi ya serikali ya Biden.

Kwa hivyo, kuna uwezekano kuwa mchakato huuo utaendelea katika siku zijazo na serikali ya Biden itajiibulia changamoto za kiusalama ikiwa ni katika kufuata mbinu ambazo hutumiwa na Warepublican kubakia madarakani na kupotosha fikra za umma.