Aug 14, 2022 02:31 UTC
  • Meli maalumu yaelekea Ukraine kuchukua nafaka kwa ajili ya nchi za Afrika

Meli ya kwanza ya kubeba nafaka imeelekea nchini Ukraine ili kuchukua ngano kwa ajili ya watu wenye njaa nchini Ethiopia. Hilo ni zoezi la kwanza la kugawa chakula barani Afrika chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuleta ahueni kwa mamilioni ya watu duniani kote walioko kwenye ukingo wa janga la njaa.

Kwa miezi kadhaa sasa vita vya Ukraine vimezuia kupelekwa nje ya nchi hiyo nafaka na bidhaa zake nyingine na hivi sasa nafaka za aina mbalimbali zimerundikana kwenye maghala, na kupeleka bei ya vyakula kupanda sana na kusababisha pia njaa barani Afrika, Mashariki ya Kati na barani Asia.

Katika siku za hivi karibuni, meli kadhaa zilizobeba nafaka zimeondoka kwenye bandari za Ukraine chini ya mkataba mpya - lakini shehena nyingi zilikuwa za chakula cha mifugo na zilikwenda Uturuki au Ulaya Magharibi.

Siku ya Ijumaa, Mkuu wa Baraza la Ulaya, Charles Michel alisema kuwa, meli ya kwanza ya kubeba nafaka kwa ajili ya watu wa Afrika ingepakia nafaka na kisha kuondoka huko Ukraine.

Meli ya kubeba nafaka 

 

Michel alisema, meli hiyo itapeleka nafaka nchini Ethiopia na ilitarajiwa kubeba zaidi ya tani 23,000, ingawa hata hivyo hiyo ni sehemu ndogo tu ya tani milioni 20 za nafaka ambazo zimerundikana nchini Ukraine.

Meli hiyo ilitarajiwa kutia nanga katika nchi ya Pembe ya Afrika ya Djibouti. Ethiopia, pamoja na nchi jirani za Somalia na Kenya, zinakabiliwa na ukame mkubwa zaidi kuwa kushuhudiwa katika kipindi cha miongo minne iliyopita.

 Maelfu ya watu wa kona mbalimbali wa ukanda huo wa Pembe ya Afrika wamekufa kutokana na njaa au magonjwa mwaka huu. Ingawa shehena moja haitakuwa na athari kubwa katika mgogoro huo, lakini Mpango wa Chakula Duniani unaendeleza juhudi za kuhakikisha hatua muhimu zaidi zinachukuliwa.