Aug 14, 2022 07:18 UTC
  • Kissinger: US ipo katika ncha ya kuingia vitani na Russia, China

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema Washington imepuuza diplomasia, na kutukuwepo kiongozi thabiti, dunia inajongelewa na vita kutokana na mizozo ya Ukraine na Taiwan.

Henry Kissinger, Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amesema hayo katika mahojiano na gazeti la Wall Street Journal na kueleza kuwa, "Tupo katika ncha ya kutumbukia vitani na Russia na China kutokana na masuala ambayo kwa kiasi fulani tuliyaibua."

Amefafanua kuwa, Marekani inataka kuitumbukiza dunia katika vita juu ya mizozo ya Ukraine na Taiwan, bila kuwa na mpango wa kujua ni vipi vita vyenyewe vitamalizika, au vitachukua mkondo gani.

Mwanadiplomasia huyo wa zamani wa Marekani mwenye miaka 99 amebainisha kuwa, Marekani hivi sasa haiwezi kuungana na China dhidi ya Russia au kuungana na Russia mkabala wa China, na inachopaswa kufanya ni kutafuta mlingano baina ya Washington, Moscow na Beijing.

US dhidi ya Russia

Kissinger ambaye ameandika kitabu kinachoeleza nafasi ya Magharibi katika mgogoro wa Ukraine ameongeza kuwa, hatua ya Russia kutuma askari nchini Ukraine mwezi Februari mwaka huu ilichochewa na usalama wake, kwa kuwa kuruhusiwa Ukraine kujiunga na shirika la kijeshi la NATO kungefanya silaha za muungano huo wa majeshi ya Magharibi zipelekewa karibu na Moscow zaidi, umbali wa kilomita 480.

Kwa mujibu wa Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia baina ya Russia na China umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika utawala wa Joe Biden, rais wa sasa wa Marekani.

Tags