Aug 14, 2022 08:44 UTC
  • Onyo la Russia kuhusu uwezekano wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Marekani

Kutokana na Marekani kuendeleza sera za uhasama dhidi ya Russia na vitisho ilivyotoa vya kuitangaza Russia nchi inayofadhili na kuunga mkono ugaidi, Moscow imeonya kuwa, kuchukuliwa uamuzi huo kutaufikisha uhusiano wa pande mbili kwenye nukta isiyorudishika nyuma na kuna uwezekano hata wa kuvunjika uhusiano wa kidiplomasia baina ya Russia na Marekani.

Alexander Darchiev, Mkuu wa Idara ya Amerika Kaskazini katika wizara ya mambo ya nje ya Russia amesema, ikiwa Seneti ya Marekai itapitisha mipango inayolenga kuitambulisha Russia kuwa nchi inayofadhili ugaidi, hatua hiyo "itasababisha madhara makubwa zaidi kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili, na kufikia hatua ya kupunguzwa au hata kuvunjwa kikamilifu".

Kwa miaka kadhaa sasa, Marekani imekuwa ikitumia silaha ya mashinikizo ikiwemo ya kuzitangaza nchi zingine au shakhsia wa nchi hizo wafadhili wa ugaidi ili kufanikisha malengo ya sera zake za nje. Ni kwa sababu hiyo, na katika mwendelezo wa mashinikizo dhidi ya Russia katika vita vya Ukraine, Washington inataka kuanzisha kampeni nyingine mpya ya kuitangaza Russia serikali inayofadhili na kuunga mkono ugaidi ili kuandaa mazingira ya kuiwekea mashinikizo makubwa zaidi nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, siku ya Jumatano iliyopita, Seneti ya Marekani ilipitisha kwa kauli moja azimio linalomtaka waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Antony Blinken aitangaze Russia nchi inayofadhili ugaidi kwa sababu ya hatua inazochukua Chechnya, Georgia, Syria na Ukraine.

 

Tangu vilipoanza vita vya Ukraine, mivutano na mikwaruzano kati ya Russia na Magharibi imeshtadi na kupamba moto. Sambamba na hilo, uhusiano wa Moscow na Washington pia umeharibika na kuvurugika sana. Hadi sasa Kremlin imeshaitahadharisha Magharibi na hasa Marekani juu ya hatua yake ya kuipelekea Ukraine silaha na zana za kivita na kusisitiza kuwa hatua hizo za Washington zitaifanya hali ya vita nchini Ukraine iwe mbaya zaidi. Hata hivyo Marekani na waitifaki wake wangali wanaendelea kuisaidia kifedha na kwa silaha Ukraine katika vita inavyopigana na Russia. Lakini pamoja na hatua zote hizo za uungaji mkono wa hali na mali unaofanywa na nchi za Magharibi kwa Ukraine, kinyume na zilivyotarajia nchi hizo, Russia ingali inasonga mbele katika medani za vita; na hatua za Wamagharibi za kuiwekea Moscow vikwazo vikali vya kisiasa na kiuchumi, si tu havijaweza kuifanya ibadilishe msimamo wake kuhusiana na Ukraine, lakini pia vikwazo ambavyo Magharibi imeiwekea Russia katika sekta ya nishati, vimekuwa na taathira hasi na mbaya kwa Ulaya badala ya Moscow.

Lakini hata nchini Marekani pia, kupanda kwa bei ya fueli na mfumuko wa bei vimeifanya nchi hiyo ionje makali ya hali ngumu ya uchumi. Pamoja na hayo, viongozi wa Washington, ambao wamegonga ukuta katika sera zao dhidi ya Russia, hivi sasa wameamua kushadidisha mashinikizo dhidi ya nchi hiyo kupitia mbinu ya kuitangaza kuwa mfadhili na muungaji mkono wa ugaidi. Kuhusiana na hilo, kitambo nyuma John Sullivan, balozi wa Marekani nchini Russia aliwahi kukiri kwa kusema: “Sisi hatuwezi katu kuvunja uhusiano kikamilifu. Hatuwezi kuvunja uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili na kutokuwa tena na mazungumzo na mashauriano yoyote yale. Ni bora wawakilishi wa nchi mbili wazungumze na kushauriana katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo. Licha ya kutofautiana, kuna ulazima kwa Marekani na Russia kuendeleza maelewano baina yao.”

John Sullivan

 

Hivi sasa, ambapo Seneti ya Marekani inafikiria kuzidisha mashinikizo dhidi ya Russia, maafisa wa Ikulu ya White House wanatahadharisha kuwa hatua kama hizo zinaweza zikawa na matokeo kinyume na yanayotarajiwa na kutoweza hasa kuiathiri Russia.

Kwa upande wao, viongozi wa Russia wametishia kuwa, endapo Washington itachukua hatua ya kuitangaza nchi hiyo mfadhili na muungaji mkono wa ugaidi hatua hiyo ya Marekani itavuka “nukta isiyoweza kurudishika nyuma.”

Ahmad Wakhshita, mhadhiri katika chuo kikuu cha urafiki wa mataifa nchini Russia analielezea hilo kama ifuatavyo: “hivi sasa uhusiano wa Russia na Marekani katika jiografia ya Magharibi umejengeka juu ya msingi wa kambi mbili kuu, huku White House ikifanya kila njia ili kurasimisha dhana ya makabiliano baina ya upande mwema na mwovu ili kurefusha kipindi cha kupooza kwa uhusiano wa Russia na Magharibi."

Hata hivyo muelekeo wa aina hiyo unaweza ukapelekea kuvunjika kikamilifu uhusiano wa kisiasa kati ya Marekani na Russia, hali ambayo haikuwahi kushuhudiwa hata vilipofikia kileleni Vita Baridi baina ya pande mbili mnamo karne ya ishirini…/

 

Tags