Aug 15, 2022 02:22 UTC
  • Kukiri Mkuu wa Sera za Nje wa EU kwamba Magharibi imeonyesha undumakuwili katika kadhia za Ukraine na Gaza

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amekiri kuwa nchi za Magharibi zinatumia vipimo vya nyuso mbili na za undumilakuwili kuhusiana na masuala ya kimataifa.

Akijibu suali aliloulizwa katika moja ya mahojiano aliyofanyiwa, kuhusu msimamo wa Umoja wa Ulaya kwa watu wa Ukraine na Gaza; pamoja na Borrell kukiri kuwa vimetumika vipimo vya aina mbili tofauti katika kuamiliana na kadhia za watu hao, ameielekezea Marekani kidole cha tuhuma hizo.

Mkuu wa sera za nje wa EU amesema: "mara nyingi tunalaumiwa kwa kutumia vipimo vya aina mbili tofauti. Lakini kwa kiwango kikubwa, siasa za kimataifa zinahusu utumiaji wa vigezo tofauti. Sisi hatutumii vipimo vya aina moja kwa ajili ya masuala yote."

Joep Borrell

 

Katika mahojiano hayo Borrell ameendelea kueleza kwamba, kuiunga mkono Ukraine dhidi ya Russia ni "ulazima wa kimaadili" kwa nchi za Magharibi. Lakini kuhusiana na hali ya Gaza, mkuu huyo wa sera za nje wa EU amesema: "kutatua masuala ya watu waliotanzika ndani ya jela ya eneo la wazi iitwayo Gaza, hakuko kwenye mamlaka ya Umoja wa Ulaya."

Ukweli ni kwamba mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya anaitakidi kuwa Magharibi inapitisha maamuzi na kuchukua misimamo kuhusiana na masuala ya kikanda na kimataifa kwa kuzingatia manufaa na maslahi yake na wala haitumii kipimo au kigezo cha aina moja tu katika masuala hayo. Kwa msingi huo, kwa kuzingatia kuwa hatua ya Russia ya kuishambulia Ukraine inahatarisha maslahi ya kimsingi ya kiusalama, kisiasa na kijiopolitiki ya nchi wanachama wa NATO, ndio maana si tu misimamo mikali kabisa imechukuliwa dhidi ya Moscow, lakini pia Ulaya imeungana na Marekani kuiwekea Russia vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa; na ili kuhakikisha nchi hiyo haishindi vita inavyopigana na Ukraine, katika kipindi hiki cha miezi sita tu tangu vilipoanza vita hivyo imeipatia serikali ya Kyiv kiwango cha juu kabisa cha misaada ya silaha na zana za kivita. Kwa mtazamo wa nchi za Ulaya ni ulazima usio na shaka kuhakikisha Russia haishindi vita dhidi ya Ukraine. Kuhusiana na hilo, Borrell amezungumzia malengo ya Ulaya katika vita hivyo kwa kusema: "Ikiwa Russia itashinda vita hivi na kukalia sehemu ya ardhi ya Ukraine, sisi waUlaya tutakuwa tumeshindwa na tutakabiliwa na tishio kubwa zaidi."

 

Huo ndio mtazamo wa mkuu wa sera za nje wa EU kuhusu "ulazima wa kimaadili" uliopo kwa nchi za Magharibi wa kuiunga mkono Ukraine. Na ndio maana Borrell anasisitiza kuwa Marekani na Umoja wa Ulaya zimekuwa na "ushirikiano mutlaki" katika kadhia hiyo.

Lakini linapokuja suala la Palestina na hasa hali mbaya ya watu wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza, ambao kwa takriban miaka 15 sasa wanateseka kutokana na mzingiro wa kila upande waliowekewa na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel, huku wakiandamwa pia kila mara na mashambulio ya kinyama ya utawala huo, mtazamo wa mambo unabadilika kikamilifu kwa Borrell kuuvua Umoja wa Ulaya jukumu na masuulia ya suala hilo na badala yake kuitupia mpira Marekani. Mkuu huyo wa sera za nje wa EU anasema: "kutatua masuala ya watu waliotanzika ndani ya jela ya eneo la wazi iitwayo Gaza, hakuko kwenye mamlaka ya Umoja wa Ulaya." Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Umoja wa Ulaya ameielezea hali ya maisha ya watu wa Gaza kuwa ni ya " kuaibisha na kufedhehesha", lakini hakuashiria chochote kuhusu chanzo cha hali hiyo mbaya ya kibinadamu.  Badala yake Borrell ametoa kisingizio cha kustaajabisha kwa kusema: "bila ya Marekani kubeba jukumu kwa uzito mkubwa hakuna njia itakayoweza kutatua mapigano haya Magharibi ya Asia".

Utawala wa Kizayuni unajulikana kuwa ni mmoja wa wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu duniani. Bila kujali sheria za kimataifa na kanuni zinazohusu haki za vita, utawala huo vamizi na mkaliaji ardhi kwa mabavu, kuanzia mwaka 2008 hadi sasa umewasha moto wa vita mara nne dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuwaua shahidi karibu watu elfu nne, robo moja ikiwa ni watoto wadogo. Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema: Ukanda wa Gaza ndio jela kubwa zaidi ya eneo la wazi duniani"

 

Haya yote yanajiri huku nchi za Ulaya zikitosheka na hatua za kidhahiri tu za kulaani kwa maneno hatua za kijinai za Israel wakati Marekani ikiamua si tu kutochukua hatua yoyote, bali kuiunga mkono Tel Aviv kikamilifu. Lakini mbali na hayo, mara kadhaa Wamagharibi wamechukua misimamo ya kuyalaani makundi ya Jihadi ya Palestina yanayokabiliana na mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni na kutaka hatua yanazochukua zikomeshwe. Nukta nyingine ni kwamba, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani ndio wadhamini wakuu wa kila aina ya silaha na zana za kijeshi ambazo utawala haramu wa Israel unazitumia kuulia Wapalestina wasio na hatia. Kwa muktadha huo tunaweza kusema kuwa, Wamagharibi ni washirika wakuu wa jinai za Israel dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.../

Tags