Aug 16, 2022 07:34 UTC
  • Ulyanov: Vikwazo dhidi ya Iran vitaondolewa karibuni

Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yao mjini Vienna, Austria amesema yumkini vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vitaondolewa karibuni hivi.

Mikhail Ulyanov, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Taasisi za Kimataifa huko Vienna ameashiria mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna na kueleza kuwa, vikwazo dhidi ya Iran huenda vikaondolewa katika muskatakabali wa karibu.

Hata hivyo mwanadiplomasia huyo wa Russia katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter amebainisha kuwa, "Siwezi kusema hayo kuhusu vikwazo dhidi ya Russia, vikwazo hivyo kwa kiasi fulani vinahusiana na (vita) Ukraine."

Ulyanov amesisitiza kuwa, Wamagharibi wanatazama sera huru ya Russia kama changamoto ya kistratajia, kwa hiyo ni muhali waachane na uraibu wao wa vikwazo.

Kutokana na ubunifu wa Iran, mazungumzo ya Vienna yameweza kupiga hatua nzuri, hata hivyo kusuasua kwa pande za Magharibi hasa serikali ya Joe Biden katika kufidia hatua haramu na za kinyume cha sheria zilizochukuliwa na serikali ya mtangulizi wake Donald Trump na kuendeleza kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa, kumeibua shaka kubwa kuhusu ukweli wa kinachodaiwa na Washington kama nia ya dhati ya nchi hiyo ya kuondoa vikwazo na kutorefusha mwenendo wa mazungumzo.

Haya yanajiri huku Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akisisitiza kuwa, endapo mistari myekundu ya Iran itazingatiwa, Jamhuri ya Kiislamu haina tatizo juu ya kufikia makubaliano; na moja ya sababu za mazungumzo kuchukua muda mrefu ni kwamba Tehran haitaki kuivuka mistari hiyo.

Tags